IQNA

Maimamu wa swala za jamaa Misri wataka al Azhar kuwa chombo huru

18:18 - April 27, 2011
Habari ID: 2113364
Kundi moja la maimamu wa swala za jamaa wa misikiti ya Misri limetoa wito wa kufanyiwa marekebisho sheria za taasisi ya al Azhar.
Kundi hilo la maimamu wa misikiti limefanya maandamano likitaka taasisi ya al Azhar kuwa chombo huru na kinachojitegemea.
Karibu maimamu elfu tatu wa misikiti ya Misri wameshiriki katika maandamano hayo yaliyoanzia katika msikiti mkuu wa al Azhar hadi kwenye ofisi za Sheikh Mkuu wa al Azhar.
Jamal Qutb mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Fatuwa ya Chuo cha al Azhar amehutubia mkusanyiko huo mkubwa wa maimamu wa misikiti ya Misri akisema kuwa matokeo ya kubanwa nafasi ya al Azhar katika kipindi cha miaka 20 ya hivi karibuni ni mashinikizo yaliyofanywa dhidi ya wanafunzi na maimamu wa misikiti, kueneza ufisadi, ugaidi na mitazamo ya kupindukia mipaka. Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 60 iliyopita wananchi wa Misri wamekuwa wakiishi katika anga iliyojaa siasa za hadaa, ghilba na hali mbaya ya kielimu. Jamal Qutb amesema katika kipindi hicho al Azhar ilikumbwa na matatizo mengi ya bajeti.
Mhadhiri wa Chuo cha al Azhar Salah Sultan pia amehutubia mjumuiko huo wa maimamu wa misikiti ya Misri akisema kuwa al Azhar inapaswa kuchukua misimamo imara ili irejeshe hadhi na nafasi yake na kuweza kutoa fatuwa kuhusu masuala mbalimbali.
Salah Sultan amesisitiza kuwa al Azhar inaweza kurejesha hadhi na nafasi yake kwa kulinda uhuru na kujitawala, kuunda baraza jipya la maulamaa na kuitisha uchaguzi wa kuainisha Sheikh Mkuu wa taasisi hiyo muhimu ya kidini. 782404
captcha