IQNA

Mashindano ya kimataifa ya Qur'ani yamvutia mtengezaji filamu Mmarekani

18:17 - April 27, 2011
Habari ID: 2113365
Mtengenezaji filamu wa Marekani Greg Barker ametengeneza filamu aliyoipa jina la "Koran by Heart" inayozungumzia kisa cha kushiriki watoto watatu katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani nchini Misri.
Kituo cha upashaji habari cha Shorouknews kimeripoti kuwa filamu hiyo inasimulia junsi watoto watatu waliohifadhi Qur'ani walivyoshiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Misri ambayo ni moja ya mashindano muhimu ya Qur'ani katika ulimwengu wa Kiislamu.
Mtengenezaji wa filamu ya Koran by Heart anasema: "Muda mrefu huko nyuma nilitaka kutengeneza filamu kuhusu ulimwengu wa Kiislamu na nilipopata habari ya mashindano ya Qur'ani ya Misri nilivutiwa mno na suala hilo na nikachukua uamuzi wa kutayarisha filamu kuhusu mashindano hayo.
Greg Barker ameongeza kuwa kinyang'anyiro hicho cha kusoma Qur'ani kina kisa cha kuvutia mno kwani kinadhihirisha sura ya kibinadamu ya dini ya Kiislamu ambayo imechafuliwa na kuharibiwa jina nchini Marekani. Amesema: "Utengenezaji filamu kuhusu mashindano ya Qur'ani yanayowashirikisha watoto wadogo umenifungulia mlango mpya."
Anasema wachezaji wakuu wa filamu hiyo ni watoto watatu wenye umri wa miaka 10 kutoka mataifa tofauti ya nje ya eneo la Ghuba ya Uajemi.
Mtayarishaji filamu huyo wa Marekani anaendelea kusimulia kwamba Uislamu haujatambuliwa ipasavyo nchini Marekani, suala ambalo ni tofauti kabisa katika eneo la Mashariki ya Kati ambako ndiyo dini kubwa zaidi na Kiarabu ndiyo lugha ya Qur'ani.
Greg Barker anamalizia kwa kusema, kuna Waislamu bilioni moja na nusu duniani na milioni mbili kati yao wanaishi Marekani. Anasisitiza kuwa Uislamu ni dini iliyoenea kote duniani.
Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Misri hufanyika kila mwaka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani yakiwashirikisha watu kutoka maeneo mbalimbali ya dunia. 782088
captcha