Kikao hicho ambacho kimekuwa kikifanyika kila mwaka mjini London kinadhaminiwa na Jumuiya ya Umoja wa Kiislamu IUF. Ajenda kuu ya kikao cha mwaka huu ni kujadili mwamko wa Kiislamu unaoonekana katika nchi nyingi za ulimwengu wa Kiislamu.
Kikao hicho ambacho kinafanyika kwa muda wa siku nne kinawashirikisha wanafikra na wanazuoni wa Kisuni na Kishia ambao wamekuwa wakisisitiza juu ya umuhimu wa kulindwa umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu kwa madhumuni ya kukabiliana na njama za maadui wa Uislamu. Wasomi hao pia wanasisitiza umuhimu wa kuzingatiwa mafundisho ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika kurejesha utukufu, izza na adhama ya ulimwengu wa Kiislamu.
Kikao cha mwaka huu cha London kimepata umuhimu mkubwa kutokana na kuwa kinafanyika katika mazingira ambayo ulimwengu wa Kiarabu unashuhudia wimbi kubwa la mwamko wa Kiislamu dhidi ya watawala dhalimu wanaotawala nchi za Kiarabu na waliopachikwa madarakani na madola ya Magharibi kwa lengo la kuhudumia maslahi ya madola hayo.
Wengi wa watu waliozungumza katika siku zilizopita za kikao hicho wamesisitiza juu ya athari kubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoanzishwa na Imam Khomeini (MA) kwa harakati na mwamko mkubwa wa Kiislamu unaoonekana hivi sasa katika nchi za Kiarabu.
Akizungumza katika kikao hicho Sheikh Muhsin Araki ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa Jumuiya ya Umoja wa Kislamu ya mjini London amesikitishwa na udhaifu mkubwa wa Waislamu katika nyanja nyingi zikiwemo za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kielimu katika karne za hivi karibuni na kusisitiza kuwa udhaifu huo ndio umepelekea kubuniwa kwa utawala haramu na wenye madhara makubwa wa Israel katika kitovu cha umma wa Kiislamu. Amesema jambo hilo limekuwa na madhara ya moja kwa moja kwa taifa la Palestina. Amesema Waislamu wote wanapasa kujifunza kutokana na msiba wa Palestina na kufahamu ni kwa kiwango gani udhaifu wao unaweza kuwasababishia madhara na misiba isiyotabirika.
Sheikh Araki ameongeza kuwa njia pekee ya kutatua matatizo ya hivi sasa ya ulimwengu wa Kiislamu ni kutegemea Qur'ani Tukufu. Amekosoa vikali uingiliaji wa Marekani katika mambo ya ndani ya nchi za Kiislamu na kuongeza kuwa nchi hiyo haina haki ya kuwatwisha Waarabu na Waislamu serikali wasizozichagua wenyewe. 811394