IQNA

Mwanafikra wa Sweden:

Itikadi ya kudhihiri Mwokozi inaonyesha haja ya kuwepo kigezo kamili

14:54 - July 16, 2011
Habari ID: 2155251
Itikadi ya wafuasi wa dini za Uislamu, Ukristo, Uyahudi na dini nyinginezo ya kudhihiri Mwokozi katika akheri zamani ni kielelezo kwamba mwanadamu anahitajia kigezo kamili.
Hayo yamesemwa na Hans Oko, mwanafikra wa Sweden anayeshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Fikra ya Umahdi unaofanyika mjini Tehran. Amesema kuwa itikadi hiyo inaonyesha kwamba wanadamu wanatafuta kitu zaidi ya kile walichonacho kwa sasa na wana matumaini ya kuwepo ulimwengu bora na kamili zaidi ambao hauwezi kufikiwa isipokuwa baada ya kudhihiri Mwokozi anayeyesubiriwa.
Hans Oko anasema kuwa itikadi ya kudhihiri Mwokozi kati ya wafuasi wa dini mbalimbali ni jambo la kuvutia kwani itikadi hiyo inabainisha kwamba wanadamu hawaridhishwi na hali inayotawala dunia ya dhulma na ukosefu wa uadilifu.
Ameongeza kuwa itikadi ya kwamba Mwokozi atakuja na kueneza uadilifu kote duniani ina maana kwamba dunia ya sasa ina mapungufu mengi yanayohitaji marekebisho. Ina maana kwamba waliodhulumiwa na kukandamizwa watarejeshewa haki zao.
Kuhusu itikadi ya mwokozi wa akheri zamani katika dini ya Kikristo, msomi huyo wa Sweden ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Mazungumzo kati ya Dini Mbalimbali wa Baraza la Kimataifa la Makanisa amesema: "Katika fikra za Kikristo, Mwokozi ambaye ni Issa Masia (as) amekwishadhihiri lakini serikali yake iliyoahidiwa bado haijaundwa na suala hilo litakamilika pale atakapodhihiri tena. Amesisitiza kuwa kuna hitilafu kati ya makundi ya Kikristo kuhusu habari za ndani juu ya jinsi ya kudhihiri kwake japo kuwa makundi yote yanaamini kwamba atakuja na kueneza amani na uadilifu kote duniani.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa madhehebu zote za Kiislamu zinakubaliana kwamba mwokozi wa ulimwengu kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume (saw) atadhihiri katika akheri zamani na kuijaza dunia, haki na uadilifu. 826245
captcha