IQNA

Historia ya chapa za kwanza za Qur'ani Ulaya katika Maonyesho ya Kimataifa ya Qur'ani, Tehran

10:57 - July 31, 2011
Habari ID: 2162440
Historia ya uchapishaji wa nakala za kwanza za Qur'ani na tarjumi ya Qur'ani Tukufu barani Ulaya inaonyeshwa kwa mara ya kwanza katika Maonyesho ya 19 ya Kimataifa ya Qur'ani mjini Tehran.
Maonyesho hayo yana nakala tofauti 40 za Qur'ani Tukufu ambazo zilichapishwa kabla ya mwaka 1857 barani Ulaya.
Baadhi ya nakala hizo zina maandishi ya Kiarabu pekee na nyingine zina tarjumi yake kwa lugha za Kiholanzi, Kijerumani, Kiingereza, Kifaransa, Kitaliano na kadhalika.
Moja ya nakala hizo za Qur'ani ina tafsiri kamili ya 'Anwarul Tanziil wa Asrarul Taawil' iliyoandikwa na Nasiruddin Abdullah bin Umar Baidhawi lakini bila ya tarjumi yake ya kilatini.
La kuvutia zaidi ni kuwa nakana nyingi zinazoonyeshwa katika maonyesho ya Tehran zimechapishwa na Wasiokuwa Waislamu na zaidi ya asilimia 90 ya watarjumi wake walikuwa Wakristo hususan wa madhehebu ya Kiprotestanti.
Majmui hiyo pia ina nakala ya kwanza ya Qur'ani iliyochapishwa mwaka 1537 Venice huko Italia na nakala iliyochapishwa mwaka 1827 mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Nakala hii ilichapishwa mjini Tabriz baada ya kuingizwa chombo cha uchapishaji nchini Iran kutoka Russia.
Maonyesho ya 19 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Tehran yaliyoanza tarehe 26 mwezi huu yataendelea hadi tarehe 26 Agosti. 833908
captcha