IQNA

Baadhi ya nchi zatangaza Jumatatu kuwa tarehe mosi Ramadhani

17:32 - July 31, 2011
Habari ID: 2162648
Baadhi ya nchi za Kiislamu zimetangaza Jumatatu Agosti mosi kuwa siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Nchi hizo ni pamoja na Kuwait, Misri, Yemen, Qatar na Imarati. Wakuu wa masuala ya kidini katika nchi hizo wamesema kuwa kufuatia kutoonekana mwezi mwandamo siku ya Jumamosi usiku, Jumapili ni siku ya mwisho ya Shaaban na siku ya Jumatatu itakuwa tarehe mosi mwezi mtukufu wa Ramadhani. Nchi kadhaa za Kiislamu ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimesema mwezi mwandamo utaanza kutafutwa leo Jumapili.
Wakati huo huo katika mahojiano na mwandishi IQNA, Kadhi Mkuu wa Kenya Sheikh Ahmad Muhdhar amesema kamati maalumu ya kutafuta mwezi mwandamo itakutana katika mji wa Mombasa leo tarehe 31 Julai ambapo itapokea ripoti za mwezi mwandamo kutoka maeneo yote ya Afrika Mashariki. Amesema iwapo mwezi utaonekana Julai 31 basi siku inayofuata itatangazwa kuwa tarehe mosi Ramadhani la sivyo siku hiyo itatangazwa kuwa tarehe 30 Shaaban.
Kadhi Mkuu wa Kenya amesema kwa miaka mingi Waislamu wa Afrika Mashariki wamekuwa wakitegemea mwezi mwandamo wa eneo hilo kuanza au kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani na hivyo amesema sera hiyo itaendelea.
834466
captcha