Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa jijini Tehran Ayatullah Muhammad Emami Kashani amesema leo kuwa, matatizo yanayoukumba ulimwengu wa Kiislamu kwa wakati huu yanatokana na Waislamu kuipuuza Qur’ani Tukufu.
Ayatullah Kashani amekumbusha kuwa Qur’an ni dira ya kumuelekeza mwanadamu kwenye kilele cha saada na ufanisi. Ameongeza kuwa, kitabu hicho cha mbinguni tena kisicho na shaka ndani yake kina uwezo mkubwa wa kunyoosha maisha ya kimaada na kimaanawi ya mwanadamu.
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa hapa Tehran amekosoa njama za Wamagharibi za kutaka kuudhalilisha Uislamu kwa kuwachukua waandishi na wasomi wa Kiislamu waliopoteza dira na itibari na kuwatumia kuandika na kuchapisha mambo yanayousawiri Uislamu kwa njia mbaya. Amewataka Waislamu kukithirisha usomaji wa Qur’ani hususan katika mwezi mtukufu wa Ramadhan. 837523