Jumuiya ya Kimataifa ya Hifdhi ya Qur'ani Tukufu, imeyaarifisha Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Dubai kuwa mashindano bora zaidi ya Qur'ani katika mwaka huu wa 2011 unaosadifiana na mwaka 1432 Hijiria.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Bayaan linalochapishwa nchini Imarati, jumuiya iliyotajwa inafungamana na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu iliyo na makao makuu yake mjini Makka.
Mashindano hayo ya Dubai yatatunukiwa zawadi maalumu ya kuyaenzi kutokana na kujipatia nafasi hiyo ya ushindi wa mashindano ya Qur'ani Tukufu. Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu imetangaza kuwa sherehe ya kuwatuza wanachama wa kamati iliyoandaa mashindano hayo ya Tuzo ya Dubai itafanyika huko mjini Jeddah Saudi Arabia hapo siku ya Alkhamisi tarehe 11 Agosti kwa usimamizi wa Mfalme Abdulla bin Abdul Aziz wa nchi hiyo.
Akizungumzia shughuli za Jumuiya ya Kimataifa ya Hifdhi ya Qur'ani, Abdullah bin Ali Baswifir, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo amesema kuwa shughuli hizo ni nyingi mno zikiwemo za kukidhi mahitaji ya wahudumu na watafiti wa Qur'ani na vilevile kuwashawishi watu wahifadhi na kuzingatia mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu.
Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tuzo ya Dubai yamekuwa yakifanyika kila mwaka nchini Imarati katika mwezi mtukufu wa Ramadhani tokea mwaka 1997. 838544