Muhammad Irani, balozi wa zamani wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Jordan amesema kuwa nchi za Magharibi zinapanga njama ya kuvunja na kudhoofisha mwamko wa Kiislamu unaoendelea katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa bara la Afrika.
Akizungumza katika Maonyesho ya Kimataifa ya Qur'ani yanayoendelea mjini Tehran, Balozi Irani amesema, mwamko huo wa Kiislamu una sifa mbili muhimu, moja ikiwa ni kasi yake kubwa ya upashaji habari na ya pili ni kuvuka mipaka ya kijiografia, jambo ambalo amesema si rahisi kuzuiwa na kitu chochote kile.
Bwana Irani amesema si sawa kuyaita matukio ya kisiasa yanayoendelea katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika kuwa ni mapinduzi kwa sababu mapinduzi yanapaswa kuleta mabadiliko ya kimsingi na ya kina katika mifumo ya tawala za nchi, hali ambayo haionekani katika mubadiliko ya kisiasa ambayo yamejiri hadi sasa katika nchi za Kiarabu. Kwa msingi huo amesema kuwa matukio hayo yanapaswa kuitwa kuwa ni mwamko wa Kiislamu.
Amesema mabadiloko hayo ya kisiasa yametokana na matakwa ya wananchi ambao wamekandamizwa kwa miaka mingi na watawala dhalimu wa nchi hizo. 844815