Mkutano huo wa siku mbili uliohudhuriwa na mamia ya wanafikra kutoka nchi za Kiislamu, Afrika, Ulaya na Marekani ulihitimishwa kwa hotuba ya Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kurejea katika izza na utukufu wa Kiislamu na kitaifa, mamlaka ya kujitawala mataifa ya Kiislamu, kusimama kidete mkabala wa mabeberu na kujikomboa kutoka katika utumwa wa kifikra, kisiasa na kiuchumi ni miongoni mwa mambo yaliyotiliwa mkazo katika taarifa ya mwisho ya mkutano huo. Taarifa hiyo imesisitiza kwamba, Waislamu wanaweza kuyafikia hayo kwa kudumisha umoja na mshikamano wao.
Sehemu nyingine ya taarifa ya mwisho ya mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Mwamko wa Kiislamu imewataka Waislamu kote ulimwenguni kuwa macho na njama za maadui, kulipa umuhimu suala la Palestina na Quds Tukufu sambamba na kuunga mkono mapambano wananchi madhulumu wa Palestina.
Imesisitiza kuwa mageuzi yanayotokea katika nchi za Kiislamu na ushindi mkubwa wa mataifa ya Waislamu umetokana na mwamko wa Kiislamu na harakati za Waislamu za kurejea katika utambulisho wao wa kidini. "Mwamko huo wa Kiislamu umeyafanya mataifa mbalimbali yasimame kidete na kuanza juhudi za kuunda serikali zilizotokana na matakwa yao wenyewe kwa mujibu wa mafundsisho ya Uislamu, yaani mfumo wa demokrasia ya Kiislamu", imesisitzia taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia imesisitiza kuwa kudumishwa harakati ya mwamko wa Kiislamu na kulindwa matunda yake kunalazimu kudumishwa mapambano dhidi ya ufisadi na ubaguzi, kulinda haki za kimsingi za raia, kufanyika jitihada kubwa za maendeleo na ustawi wa kiuchumi kupitia sera za kupambana na umaskini, kustawisha uwekezaji, kulea kizazi kipya cha wasomi wanaoishikamana barabara na mafundisho ya Uislamu na kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi za Kiislamu.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesisitiza kuwa hitilafu katika safu za wanamapinduzi, mapigano ya kikaumu, kikabila na kimadhehebu na ugomvi wa mipaka vinadhoofisha umma wa Kiislamu na kuwapa maadui fursa ya kutekeleza njama zao dhidi ya Waislamu; kwa msingi huo kuna udharura wa watu wote hususan viongozi wa harakati za Kiislamu kutambua tofauti zao na kuziongoza kwa njia ya busara ili kuepuka mitego ya aina hiyo, kukufurishana na kadhalika. Vilevile imeishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uongozi wenye busara wa Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khameni ambaye imesema, daima amekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mwamko wa Kiislamu na kulinda dini hiyo tukufu na wafuasi wake. 863411