IQNA

Katibu Mkuu wa Muungano wa Maulamaa wa Kiislamu Duniani:

Mageuzi yanayofanyika katika nchi za Kiarabu ni bishara njema ya kukombolewa Palestina

10:56 - October 02, 2011
Habari ID: 2197080
Katibu Mkuu wa Muungano wa Maulamaa wa Kiislamu Duniani amesema kuwa mageuzi yanayofanywa na wananchi katika nchi za Kiarabu yamefupisha masafa ya kukombolewa Quds Tukufu na yanatoa bishara njema ya kukombolewa Palestina.
Ali Qaredaghi ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa tano wa kimataifa wa kuunga mkono mapambano ya Intifadha ya wananchi wa Palestina unaofanyika mjini Tehran amesema kuwa Palesina ndiyo kadhia muhimu zaidi ya umma wa Kiislamu, na mwamko wa sasa wa umma wa Kiislamu umekuwa na taathira katika juhudi za kutetea haki za Wapalestina. Ameongeza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ulighusubu ardhi za Palestina kwa msaada wa ubeberu wa kimataifa hususan Uingereza na Ufaransa lakini leo hii utawala huo unadhoofika siku baada ya siku kwa sababu dhulma haidumu na uvamizi utatoweka na kuangamizwa.
Ali Qaredaghi mesisitiza kuwa mazungumzo ya mapatano kati ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni yameshindwa, hivyo wakati umefika kwa umma wa Kiislamu kupambana na Israel kwa ajili ya kuzikomboa ardhi za Palestina.
Sheikh Ali Qaredaghi ameongeza kuwa, Palestina ndiyo kadhia muhimu zaidi ya umma wa Kiislamu na kwamba ugomvi mkubwa uliopo baina ya Waislamu na Wazayuni maghasibu ni suala la Palestina.
Amesema, Palestina ni kielelezo cha mwamko, nguvu, umoja au udhaifu na kubaki nyuma umma wa Kiislamu na amezitaka nchi zote za Kiislamu kufanya idili ya hali ya juu ya kujiletea maendeleo na kuunga mkono haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kustafidi kwa njia za amani na teknolojia ya kisasa ya nyuklia.
Aidha amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, taifa na serikali ya Iran kutokana na uungaji mkono wao wa dhati kwa taifa la Palestina na kuongeza kuwa, Muungano wa Maulamaa wa Kiislamu Duniani daima utaendelea kuunga mkono mapinduzi ya wananchi katika nchi za Kiarabu na unaamini kuwa ukombozi wa Palestina utawezekana pale tu mataifa ya Kiarabu na Kiislamu yatakapojikomboa. 871139

captcha