Ali Jumu'a, Mufti wa Misri amesema kuwa wimbi jipya la mashambulio yanayotekelezwa na walowezi wa Kizayuni dhidi ya matukufu ya Kiislamu ni ishara ya wazi inayothibitisha uongo wa utawala wa Israel kwamba unaheshimu matukufu ya Waislamu na Wakristo.
Katika kutoa radiamali yake kuhusiana na mashambulio yaliyofanywa hivi karibuni na walowezi wa Kiyahudi dhidi ya makaburi ya Waislamu na Wakristo katika mji wa Yafa, Mufti huyo wa Misri ametoa taarifa akiyalaani vikali na kusema kuwa hiyo ni ishara ya wazi inayothibitisha uongo wa utawala haramu wa Israel kwamba unaheshimu matukufu ya dini mbili hizo za mbinguni. Ametaka kutiwa nguvuni na kuhukumiwa wahalifu wote waliohusika na kitendo hicho cha kinyama na cha aibu. Amesema kitendo hicho kinachokwenda kinyume na misingi na maazimio ya kimataifa kinapaswa kukemewa na dini zote za mbinguni.
Mufti wa Misri amewataka Waislamu na Waarabu kusimama na kutoa mashinikizo dhidi ya utawala haramu wa Israel ili usimamishe mara moja njama zake za kufuta alama za Kiislamu na Kikristo katika mji mtakatifu wa Quds. Ameyataka pia makundi yote ya Palestina kukabiliana na njama hizo hatari za Wazayuni kwa kuimarisha umoja na mshikamano kati yao.
Siku ya Jumamosi iliyopita Mayahudi wenye misimamo ya kupindukia mipaka waliingia kwenye makaburi ya Waislamu na Wakristo huko katika mji wa Yafa na kuharibu makaburi 22 ya Waislamu na Manne ya Wakristo.
Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita pia, Wazayuni wamekuwa wakiharibu na kuteketeza moto misikiti ya Waislamu na sasa inaonekana wazi kuwa kuvunjiwa heshima makaburi yao ni aina mpya ya dharau na ukosewaji heshima matukufu ya Waislamu unaofanywa na walowezi wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa watawala wa Tel Aviv. 876817