IQNA

Askofu wa Wamaroni wa Lebanon ataka kutolewa mashinikizo dhidi ya utawala wa Kizayuni

17:25 - October 24, 2011
Habari ID: 2211037
Bashara ar-Rai, Askofu Mkuu wa Wakristo wa Kimaroni wa nchini Lebanon jana Jumapili alizungumza huko New York nchini Marekani na kuutaka Umoja wa Mataifa utekeleze kisheria majukumu yake kuhusiana na suala la Palestina na kutoa mashinikizo zaidi dhidi ya utawala haramu wa Israel.
Bashara ambaye alionana na kuzungumza hiyo jana Jumapili na Ban Ki Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo na taasisi nyingine za kimataifa zinapasa kutekeleza vyema majukumu yao kuhusiana na suala la Palestina ndipo zitarajie Hizbullah kuchukua hatua ya kuweka chini silaha zake.
Amesema huenda suala la silaha za Hizbullah likachukuliwa na taasisi za kimataifa kuwa jambo muhimu lakini akaongeza kwamba kabla ya jambo hilo taasisi hizo zinapasa kwanza kutoa mashinikizo dhidi ya utawala haramu wa Israel ili uondoke katika ardhi za Wapalestina na kuruhusu wakimbizi wa Kipalestina warejee katika ardhi zao.
Askofu Mkuu huyo amesema katika sehemu nyingine ya matamshi yake kwamba jamii ya kimataifa inapasa kufanya juhudi za kupatanisha vyama vya kisiasa vya Lebanon ili viweze kuimarisha umoja wa kitaifa nchini.
Amesema kupatikana amani katika Mashariki ya Kati kunahitajia masuala mawili nayo ni ya kuondoka utawala haramu wa Israel katika ardhi za Wapalestina na kuruhusu wakimbizi wa Palestina warejee katika ardhi zao. Katika safari yake ya siku tatu nchini Marekani, Askafu ar-Rai atakutana na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa kisiasa, kidini na wawakilishi wa nchi tofauti nchini humo. 885927
captcha