Ujumbe uliotolewa na katibu mkuu huyo unasema kuwa leo hii umma wa Kiislamu unahitajia umoja na mfungamano kuliko wakati mwingine wowote kwa madhumuni ya kufikia utukufu wa Kiislamu na hasa kuhusiana na suala la Quds Tukufu na kutatuliwa suala la Palestina.
Ekmeleddin Ihsanoglu amesema kwenye ujumbe huo kwamba kwa mara nyingine tena OIC inaunga mkono kwa dhati juhudi za Palestina za kupewa uanachma kamili katika Umoja wa Mataifa na kwamba itaendeleza juhudi zake katika uwanja huo.
Katika sehemu nyingine ya ujumbe huo Katibu Mkuu wa OIC ameashiria hali ya kusikitisha ya njaa na ukame nchini Somalia na kutaka Waislamu wasiwasahau Waislamu wenzao wa Afrika na wakati huohuo kuzishukuru nchi ambazo hadi sasa zimejitolea katika kuwafikishia Waislamu wa nchi hiyo msaada wa dharura.
Ameashiria pia matukio ya nchi nyingine za Kiislamu na kusema kuwa matukio hayo yanaonyesha umuhimu wa kuzingatiwa sheria na haki za binadamu katika kuleta amani na utulivu katika nchi hizo. Amesema kwamba ana matumaini kuwa matukio hayo ambayo yametokea katika nchi za Tunisia, Misri na Libya yataleta demokrasia na ustawi wa Kiislamu kwa maslahi ya Waislamu katika nchi hizo. 892906