IQNA

Rais Ahmadinejad akabidhi sheria ya kupunguza uhusiano na Uingereza

23:52 - December 07, 2011
Habari ID: 2235033
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekabidhi sheria ya kupunguza uhusiano wa Iran na Uingereza kwa ajili ya utekelezaji.
Sheria ya kupunguza uhusiano wa Iran na Uingereza ilipasishwa hivi karibuni kwa kura nyingi katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran na kupitishwa pia na Baraza la Kulinda Katiba la Iran kabla ya kupelekwa kwa Rais Ahmadinejad kwa ajili ya kutekelezwa.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, sasa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ina muda wa wiki mbili kuhakikisha kuwa imepunguza uhusiano wa kisiasa wa Tehran na utawala wa kifalme ya Uingereza ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia hadi kufikia balozi mdogo.
Sheria hiyo pia inataka uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa Iran na Uingereza upunguzwe sana na kufikia kiwango cha chini kabisa.
Hatua hiyo ya Iran imechukuliwa ili kulinda manufaa ya taifa na haki za wananchi Waislamu wa nchi hiyo ambao wana uzoefu mchungu na siasa za kikoloni za mkoloni mkongwe Uingereza.
Hatua ya Bunge la Iran ya kupitisha muswada wa kupunguza uhusiano wa Tehran na London imeikasirisha sana serikali ya kifalme ya Uingereza kiasi kwamba imeamua kuchukua hatua za pupa za kufunga ubalozi wa Iran mjini London jambo ambalo Tehran inasema haliwezi kuteteresha hata kidogo msimamo wake wa kupunguza uhusiano na utawala wa kikoloni wa ufalme wa Uingereza.
911707
captcha