Rais Al-Munsif al-Marzouqi wa Tunisia amesema kuwa ushindi wa Waislamu katika chaguzi za nchi hiyo, Misri na Morocco zinaonyesha jinsi mataifa ya Kiislamu yalivyo na imani kwamba Uislamu ndio suluhisho la pekee la matatizo yao.
Al-Marzouqi aliyasema hayo siku ya Jumanne alipoonana na kuzungumza na Mustafa Abdul Jalil Mkuu wa Baraza la Mpito la Libya huko Benghazi. Amesema utambuzi wa wananchi kwamba mafundisho ya Kiislamu ndiyo njia bora ya utatuzi wa matatizo na changamoto zinazowakabili ndiyo sababu kuu iliyopelekea Waislamu wapate ushindi mkubwa katika nchi za Misri, Tunisia na Morocco.
Amesema Waislamu ambao wameweza kuwang'oa madarakani madikteta wa nchi hizo kwa kutegemea imani yao, wanatambua vyema kwamba Uislamu unaweza kuwa suluhisho bora la kutatua matatizo ya zama hizi na ndio maana wakawachagua watu walio na misimamo ya Kiislamu kuwaongoza.
Rais huyo mteule wa Tunisia ambaye alikuwa mpinzani wa muda mrefu wa dikteta Zeinul Abidin aliyeng'olewa madarakani nchini humo amesisitiza kwamba vyama vya Kiislamu vilivyoshinda katika chaguzi za nchi zilizotajwa havipingi hata kidigo uhuru wa wananchi walioupata baada ya kung'olewa madarakani tawala za kidikteta za nchi hizo.
Ameongeza kuwa vyama vya Kiislamu vinapaswa kupewa fursa ya kutawala na kutowekewa vikwazo katika uwanja huo. 928982