Kwa mujibu wa tovuti ya Muslim Village, Arsalan Bukhari, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Uhusiano wa Uislamu na Marekani mjini Washington amesema kwamba maandamano hayo ambayo yamepangwa na baraza hilo kufanyika tarehe 16 mwezi huu wa Januari yatafanyika chini ya anwani ya Siku ya Waislamu wa Jimbo la Washington katika Congress.
Waandaaji wa maandamano hayo wanasema kuwa yatawashirikisha zaidi ya Waislamu 400 ambao watakutana na kufanya mazungumzo na wabunge wa Marekani. Wanasema hiyo itakuwa ni fursa nzuri kwa Waislamu kufahamu mwenendo wa sheria za Marekani na vilevile kukutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wao bungeni.
Waandamanaji watawakabidhi wabunge hao nakala za Qur'ani zilizotarjumiwa kwa Kiingereza na kuwataka wabuni sheria za kupambana na tatizo la ongezeko la chuki na jinai dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Idadi ya Waislamu wa Marekani inakisiwa kuwa kati ya watu milioni 6 hadi 8. Jamii hiyo imekuwa ikikabiliwa hivi karibuni na ongezeko kubwa la chuki na uadui kutoka kwa maadui wa Uislamu. 932197