Leon Panetta Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameto taarifa akiwaomba radhi Waislamu wa Afghanistan kutokana na kitendo cha askari jeshi wa nchi hiyo cha kukivunjia heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu, Qur'ani Tukufu, katika kambi yao ya kijeshi ya Bagram.
Waziri huyo amelazimika kuwaomba msamaha Waislamu wa Afghanistan kutokana na kukasirishwa kwao na kitendo cha askari wa Marekani cha kuchoma moto nakala kadhaa za Qur'ani Tukufu. Akiashiria msamaha uliokuwa umeombwa awali na Jenerali John Allen, Kamanda wa kikosi cha Nato nchini Afghanistan kutokana na kitendo hicho cha dharau dhidi ya matukufu ya Kiislamu, Waziri Panetta amedai kwamba kitendo hicho hakiakisi msimamo wa jeshi la Marekani kuhusiana na matukufu hayo.
Ameendelea kudai kwamba Marekani inaheshimu thamani na itikadi zote za kidini za watu wa Afghanistan na kuahidi kwamba jeshi la Marekani litafuatilia na kuwaadhibu wale wote waliohusika na kitendo hicho ili kuzuia kukaririwa tena.
Wananchi wa Afghanistan jana Jumanne walifanya maandamano makubwa mbele ya kituo cha kijeshi cha Marekani mjini Kabul kulalamikia kitendo hicho cha askari wa Marekani cha kuchoma moto Qur'ani Tukufu. 958136