Taarifa ya Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bayt AS imesema, katika kipindi hiki ambacho Waislamu duniani wameanza kutumia mbinu mpya kutekeleza mafundisho ya Qur'ani Tukufu, wameanzisha mwamko wa Kiislamu na wanawaangusha vibaraka wa shetani mmoja baada ya mwingine, sasa madola adui yameanza kuonyesha uhasama dhidi ya mwamko huo.
Vikosi vamizi vya Marekani huko Afghanistan havijatosheka na jinai ya kuivamia nchi hiyo na kuwaua maelfu ya watu wasio na hatia bali sasa wanajeshi hao vamizi wameteketeza moto Qur'ani Tukufu na vitabu vingine vya kidini katika kituo cha kijeshi cha Bagram.
"Hatua hii inaenda sambamba na njama ya mhubiri mwendawazimu wa Kikristo wa Marekani (ambaye aliteketeza moto nakala ya Qur'ani)", imeongeza taarifa hiyo.
Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bayt AS imesema: "Kuvunjia heshima matukufu ya kidini ni hatua ya kijahili na isiyo ya kimantiki ambayo inapaswa kulaaniwa na watu wote huru na wenye imani halisi kutoka dini zote".
Jumuiya hiyo imesema Waislamu wa dunia wanaionya vikali Marekani na vibaraka wao wasikariri vitendo kama hivyo vya kishenzi.
Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bayt AS pia imetoa wito kwa serikali ya Afghanistan kuchukua hatua za kivitendo kuzuia hatua hizo za kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu. 'Hatua ya kwanza ni kuhakikisha vikosi vamizi vya majeshi ya kigeni vinaondoka Afghanistan', imesema taarifa hiyo.
Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bayt AS imetoa wito wa taasisi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, UNESCO, OIC pamoja na serikali za Kiislamu kukabiliana kisheria na kitendo hicho cha kishenzi cha wanajeshi wa Marekani.
Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bayt AS pia imewataka Waislamu duniani kulipa umuhimu na uzito mkubwa suala la Umoja wa Kiislamu kwani maadui wa Uislamu na madola ya istikbari duniani hayatathubutu kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu iwapo Waislamu wameungana.
958722