IQNA

Kiongozi Muadhamu awashukuru wananchi wa Iran kwa kushiriki katika uchaguzi

10:11 - March 10, 2012
Habari ID: 2288458
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislam amewashukuru wananchi wa Iran kwa dhati kutokana na harakati yao adhimu, ya wakati unaotakiwa, ya kupevuka kisiasa na yenye muono wa mbali ya kujitokeza kwa wingi mno katika uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran uliofanyika hivi karibuni
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa shukrani hizo Alkhamisi Machi 8 mjini Tehran aliponana na mkuu pamoja na wajumbe wa Baraza la Wataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu.
Kiongozi Muadhamu mebainisha taathira na ujumbe mkubwa unaopatikana kutokana na kujitokeza kwa wingi mno wananchi wa Iran katika uchaguzi huo akisisitiza kuwa, kura za wingi mutlaki za wananchi katika uchaguzi wa Bunge la Tisa (la Jamhuri yaKiislamu ya Iran) kwa hakika ni kuupigia kura ya ndio Mfumo wenyewe wa Kiislamu nchini na zinaonesha jinsi wananchi wanavyouamini kikamilifu mfumo wao wa utawala na vile vile ni mithili ya kibao cha uso cha kuwaamsha na kuwatanabahisha wale watu ambao wamelala kwenye usingizi mzito wa fikra na mawazo potofu kuhusiana na mfumo huu na ambao bado wana ndoto dhidi ya mfumo huu. Amesema hilo ni pigo kubwa kwa watu hao la kuwafanya waamke na wauone uhakika wa mambo ulio wazi.
Kiongozi Muadhamu pia amesisitiza kwamba wananchi azizi wa Iran wametimiza hoja kikamilifu kupitia uchaguzi huo na kuongeza kuwa, katika uchaguzi wa Machi 2, wananchi wa Iran walionesha nguvu zao zinazotokana na imani na muono wa mbali katika mapambano na kambi ya wapinzani na kwa harakati yao hiyo adhimu, wananchi hao wameweza kuishinda na kuifelisha mipango ya miezi mingi ya maadui wenye chuki na inadi kubwa ambao walitaka, kupitia njama zao hizo, wawafanye wananchi wa Iran wasijitokeze katika uchaguzi huo.
Ayatullahil Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, kujitokeza kwa wingi mkubwa wananchi katika uchaguzi huo kwa hakika kumeonesha kuendelea kumiminika rehema za Mwenyezi Mungu kwa Iran na ni kwa sababu hiyo ndio maana tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuleta sijda ya shukru kutokana na rehema hizo za Mwenyezi Mungu.
Amesema, rehema za Mwenyezi Mungu inabidi ziandaliwe mazingira ya kushuka kwake na kuongeza kuwa: Kutokana na kujitokeza katika medani, na kutokana na muono wake wa mbali na kusimama kwake imara, taifa la Iran limeandaa mazingira ya kushukiwa na rehema za Mwenyezi Mungu na inabidi kumshukuru Mwenyezi Mungu sana kutokana na kupatikana taufiki hiyo.
Aidha kwa mara nyingine Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwa kusema: Ninawashukuru wananchi azizi wa Iran kwa udhati wa moyo wangu.
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei amewashukuru wahusika na maafisa wote walioendesha uchaguzi wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Kiislamu na hasa Baraza la Kulinda Katiba kutokana na jukumu zito na nyeti walilochukua na kuongeza kwamba: Katika uchaguzi huu, Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wakuu na vyombo vya usalama, vyombo vya utangazaji, Shirika la Redio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu vyombo vyote kwa hakika vimefanya kazi kubwa na muhimu mno na vimeweza kufanikisha jambo hilo muhimu sana, kwa njia iliyo bora kabisa.
Baada ya hapo amegusia jinsi demokrasia ya kidini ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivyo kigezo kwa mataifa mengine na jinsi uchaguzi ulivyo muhimu sana nchini akisema: Uchaguzi ni nguzo muhimu sana kwa Mfumo wa Kiislamu na kwamba demokrasia ya kidini inategemea uchaguzi hivyo kila mtu ambaye ana imani na Mfumo wa Kiislamu nchini, analihesabu suala la kushiriki katika uchaguzi kuwa ni jukumu lake na hata kama atakuwa anakosoa baadhi ya mambo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, watu wote walioshiriki kwenye uchaguzi wa siku ya Ijumaa (Machi 2, 2012) kwa kweli sambamba na kutekeleza wajibu wao, wameonesha pia ufahamu wao sahihi kwani katika mfumo wa demokrasia ya kidini, mtu hapaswi kususia uchaguzi kwa sababu tu haridhishwi na baadhi ya mambo.
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha pia taathira za uchaguzi huo wa Machi 2 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kusisitiza kuwa, uchaguzi huo ulikuwa mithili ya kibao (cha uso) cha kuwaamsha wale watu ambao wamelala kwenye njozi na fikra potofu kuhusiana na Mfumo wa Kiislamu na kuhusiana na wananchi wa Iran na kwamba uchaguzi huo umewazindua watu hao na kuwawekea wazi uhakika wa mambo mbele ya macho yao.
Aidha amegusia matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani aliyedai kuwa yeye hana mawazo kabisa ya kuingia vitani na Iran na kuongeza kuwa, matamshi hayo ni matamshi mazuri na yanaonesha kuwa amezinduka kutoka usingizini, lakini Rais wa Marekani wakati huo huo amesema wana nia ya kutumia vikwazo kuwapigisha magoti ya utii wananchi wa Iran ambapo sehemu hiyo ya matamshi yake inaonesha kuwa bado amezama katika ndoto.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kitendo cha kuendelea na njozi hizo ni pigo kwa viongozi wa Marekani na ni jambo lisilo na shaka kuwa mahesabu yao yatafeli tu kwani kambi ya maadui wa Iran wenye chuki na inadi, na hasa Marekani, kwa zaidi ya miaka 33 sasa wameliwekea vikwazo taifa la Iran na kushadidisha zaidi vikwazo hivyo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kama njia ya kuwafanya wananchi wa Iran wakae mbali na Mfumo wao wa Kiisalmu lakini watu wote wameona jinsi wananchi wa Iran walivyojitokeza kwa wingi sana katika uchaguzi wa Machi 2 na kuwathibitishia kivitendo watu wote jinsi walivyoshikamana vilivyo na utawala wao wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, nukta nyingine muhimu katika uchaguzi wa siku ya Ijumaa ni jinsi wananchi wa Iran walivyoweza kuonesha namna wanavyouamini Mfumo wa Kiislamu.
Ameongeza kuwa, baada ya uchaguzi wa Rais wa mwaka 2009, baadhi ya watu walikuwa wanatabiri kwamba wananchi wa Iran hawana imani tena na utawala wao na kwamba wangelisusia uchaguzi wa Bunge wa Machi 2, 2012, lakini fikra hiyo imethibitika kuwa ilikuwa ghalati na isiyo na ukweli hata kidogo.
Amekumbusha kuwa, ijapokuwa uchaguzi wa siku ya Ijumaa (Machi 2) ulikuwa ni uchaguzi wa Bunge, lakini kila kura ya wananchi kwa hakika ilikuwa ni kura kwa Mfumo wa Kiislamu na hatua ya wananchi wa Iran ya kujitokeza kwa wingi mutlaki katika masanduku ya kupigia kura na hivyo kuweka rekodi nyingine mpya ya kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi katika kipindi hiki cha miaka 33, ni jambo linaloonesha kwamba wananchi wana imani kamili na Mfumo wao wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuwa na muono wa mbali na kupevuka kifikra wananchi wa Iran kuwa ni nukta nyingine muhimu iliyojitokeza katika uchaguzi wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, wananchi wote, kuanzia wale ambao hii ilikuwa ni mara yao ya kwanza kupiga kura au wale wazee ambao tayari wameshashiriki mara nyingi katika uchaguzi, wote walikuwa na sababu zao zilizowavutia kushiriki kwenye uchaguzi huo na sababu muhimu zaidi ni kwamba wameona kuwa adui anaivizia nchi yao, na taifa lao linaandamwa na mashambulizi ya kambi ya maadui wenye chuki na inadi, jambo ambalo kwa kweli linaonesha jinsi wananchi wa Iran walivyo macho na walivyo na muono wa mbali.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, nukta nyingine inayohusiana na uchaguzi huo ni jukumu kubwa lililo nalo Bunge lililochaguliwa kwenye uchaguzi kama huo na kwamba watu wote waliochaguliwa na wananchi wanapaswa kutambua kuwa wana majukumu makubwa ikiwa ni pamoja na kutunga sheria zenye faida kubwa kwa kutumia busara na umakini wa hali ya juu.
Vile vile ameashiria jukumu la Bunge la kupitisha Mawaziri na suala zima la kushiriki katika kuundwa serikali mbali mbali nchini na kukumbusha kuwa, katika kutekeleza jukumu lake hilo, Bunge linapaswa kuwa na umakini kama ambavyo linapaswa pia kuwa na insafu na uadilifu na si sahihi kuzingatia umakini tu na kukosa kuwa na insafu na uadilifu.
Vile vile ameusia kufanyika kazi kwa werevu na ikhlasi na kuongeza kuwa, ajenda kuu ya viongozi wote wa mihimili mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) inapaswa iwe ni kufanya kazi kwa ikhlasi na kwa kutekeleza vizuri majukumu na vile vile wachunge sana umaanawi na mafundisho ya dini katika vyeo vyao.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa fremu na kitu kinachopambanua mambo katika mfumo wa demokrasia ya kidini ni uchaguzi na kura za wananchi na kusisitiza kuwa, marejeo makuu ya mfumo wa demokrasia ya kidini ni Uislamu na jambo hilo halipaswi kufumbiwa macho hata kidogo.
Ameongeza kuwa, Uislamu unaweza kuiletea nchi heshima, utukufu, maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, maendeleo ya kimaadili, malengo matukufu na kuonesha njia bora za kuweza kufikia malengo hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, demokrasia katika mfumo wa demokrasia ya kidini chimbuko lake ni Uislamu na kukumbusha kuwa, kama kuna watu wanadhani kwamba demokrasia chimbuko lake ni nchi za Magharibi basi wajue wanakosea kwani ijapokuwa muundo wa demokrasia katika mfumo wa Kiislamu na mifumo ya Magharibi unafanana, lakini viini na chimbuko lake linatofautiana.
Amesisitiza kuwa, mfumo wa demokrasia ya kidini unahesabu kura za wananchi kuwa zina utukufu na heshima kubwa na kuongeza kuwa, misingi na fremu za mfumo wa demokrasia ya kidini zinatofautiana kikamilifu na fremu za demokrasia ya nchi za Magharibi kwani demokrasia ya Magharibi imesimama juu ya misingi ya dhulma.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua zaidi kuhusu misingi ya dhulma iliyosimama juu yake demokraisa ya nchi za Magharibi na kusema kuwa, nchi hizo zinalihesabu kuwa ni kosa na uhalifu suala la kukana au kutilia shaka tu ngano ya Holocaust na wakati huo huo lakini, nchi hizo za Magharibi zinasema kuwa mtu hana haki ya kulalamikia kuvunjiwa heshima wazi wazi Mtume Muhammad SAW. Amesema huo ni moja ya mifano ya wazi ya jinsi misingi ghalati na ya kidhulma inavyotawala demokrasia ya nchi za Magharibi.
Amesema, mfano mwingine wa dhulma hiyo ni jinsi demokrasia ya nchi za Magharibi inavyopiga marufuku wanawake wanaovaa vazi la staha la Hijabu kwenda makazini na mavazi yao hayo ya heshima.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, katika mfumo wa demokrasia ya kidini lakini, sharia, dini na hukumu za Mwenyezi Mungu ni lazima zitekelezwe na zinahesabiwa kuwa ndio msingi wa maisha ya mtu binafsi na jamii kiujumla.
Ameongeza kuwa, katika mfumo huo, masuala yote, iwe ni kuchagua watu wa kutunga sheria, au watekelezaji wa sheria, majukumu yote ya kufanya hivyo yako mikononi mwa wananchi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya juhudi zake zote kuhakikisha kuwa misingi hiyo inatekelezwa vilivyo kwa namna ambayo Uislamu umeamrisha.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Mahdavikani, Mkuu wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu ametoa hotuba fupi na sambamba na kuwashukuru wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Bunge wa Machi 2, 2012, amesema kuwa, miongozo iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imetoa mchango mkubwa sana katika kufanikiwa hamasa hiyo na kuongeza kuwa, moja ya nguzo kuu za Mapinduzi na Mfumo wa Kiislamu nchini Iran, ni kujitokeza vilivyo wananchi katika medani mbali mbali jambo ambalo lilikuwa linasisitizwa mara kwa mara na Imam Khomeini (quddisa sirruh).
Ayatullah Mahdavikani amesisitiza pia kuwa kulindwa na kuendelea kuimarika Mfumo wa Kiislamu nchini Iran kunategemea kulindwa na kuhifadhiwa nguzo zake yaani Wilaya na nafasi ya Kiongozi Muadhamu na kuongeza kuwa, wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu wanaheshimu kikamilifu ahadi waliyofunga na Kiongozi Muadhamu na wanaliheshabu suala la kulinda nafasi ya Kiongozi Muadhamu na Fakihi Mtawala kuwa ni jukumu na wajibu wao.
Vile vile katika mkutano huo, Ayatullah Yazdi, Naibu wa Mkuu wa Baraza la WanazuoniWataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti kuhusu masuala yaliyojadiliwa katika kikao cha siku mbili zilizopita cha baraza hilo.
968046

captcha