IQNA

Wabahrain wanataka demokrasia ya kweli

10:23 - March 10, 2012
Habari ID: 2288479
Wananchi wa Bahrain watafanya kila wawezalo ili kuhakikisha kuwa demokrasia ya kweli inapatikana nchini humo.
Haya ni kwa mujibu wa Mkuu wa chama kikuu cha upinzani Bahrain cha Al Wefaq Sheikh Ali Salman.
Akihutubia halaiki kubwa ya wananchi wanaoupinga utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa siku ya Ijumaa, Sheikh Salman amepongeza azma na irada imara ya watu wa Bahrain hasa wanawake ambao wamejitolea muhanga kutetea uhuru kamili wa nchi yao.
Sheikh Salman ametoa wito wa kufanyika kura ya maoni ili kutatua mgogoro wa muda mrefu wa Bahrain.
Wakati huo huo maelfu ya wananchi wa Bahrain Ijumaa ya jana walifanya maandamano makubwa ya kupinga serikali katika mji mkuu Manama, na kutaka utawala wa Aal Khalifa uondoke madarakani. Waandamanaji hao sambamba na kutoa nara mbalimbali wametaka kupinduliwa utawala wa kidhalimu wa kifalme wa Bahrain.
Saeed al-Shahabi Mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Bahrain amesema katika maandamano hayo kuwa utawala wa Aal Khalifa ni tezi la saratani ambalo linapaswa kuondolewa.
Baadhi ya duru za habari zimeripoti kuwa zaidi ya nusu ya wananchi wa Bahrain wameshiriki katika maandamano hayo makubwa ya Ijumaa.
Wakati hayo yakiripotiwa wananchi wa Iraq nao pia siku ya Ijumaa waliandamana katika miji tofauti ya nchi hiyo kuunga mkono mapinduzi ya wananchi wa Bahrain. Taarifa zinasema kuwa wafuasi wa kundi la Sadr wameandamana katika miji tofauti ya Iraq baada ya mshuko wa Sala ya Ijumaa na kuunga mkono mapinduzi ya wananchi wa Bahrain.
Kiongozi wa kundi hilo Muqtada Sadr siku kadhaa zilizopita aliitisha maandamano hayo na kuvitaka vikosi vamizi vya Saudi Arabia viondoke nchini Bahrain.
968324
captcha