
Katika mfululizo wa mazungumzo ya simu na viongozi wa nchi mbalimbali za Kiislamu katika mkesha wa siku kuu ya Eid al-Adha, Rais Pezeshkian amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa Kiislamu na kupanua ushirikiano wa kikanda.
Katika mazungumzo na Rais wa Kyrgyzstan, Sadyr Japarov, Rais Pezeshkian amesema Eid al-Adha ni alama ya imani, mshikamano, na umoja miongoni mwa mataifa ya Kiislamu. Aidha, ametoa shukrani kwa Kyrgyzstan kwa kupinga azimio la hivi karibuni la kupinga Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akiilitaja hatua hiyo kuwa dhihirisho la “mahusiano ya kirafiki, kuheshimiana, na msimamo huru na wa kuwajibika” katika masuala ya kimataifa.
Katika mazungumzo tofauti na Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi, Rais Pezeshkian amesema kuwa eneo hili litashinda mivutano ya sasa ambayo imechochewa na vitendo vya pamoja vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Rais Pezeshkian amesisitiza tena azma ya Iran ya kutumia njia za kidiplomasia na majadiliano katika kutatua masuala ya kikanda, akibainisha kuwa operesheni za hivi karibuni za kulipiza kisasi dhidi ya kambi za Marekani katika eneo zilitekelezwa ndani ya mfumo wa haki halali ya kujihami.
Katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim, Rais wa Iran amesema kuwa umoja miongoni mwa ulimwengu wa Kiislamu unaweza kuwezesha hatua za pamoja za kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni na Marekani. Alipongeza msimamo wa Malaysia dhidi ya vitendo haramu vya Marekani na Israel katika eneo hilo na amemshukuru Anwar kwa juhudi zake za kukuza amani ya kimataifa.
Rais Pezeshkian pia amefanya mazungumzo na Rais wa Iraq, Nizar Amidi, na Waziri Mkuu, Ali Falih al-Zaidi, akieleza Eid al-Adha kama alama ya kujitolea, umoja, na udugu miongoni mwa mataifa ya Kiislamu. Vilevile, amezungumza na Rais wa Tajikistan, Emomali Rahmon. Rais wa Iran amesmshukuru Rais Rahmon kwa maneno yake ya faraja kufuatia uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Katika mazungumzo ya simu na Amiri wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Rais Pezeshkian amesema kuwa Tehran iko tayari kutafuta “utaratibu wa heshima” ili kumaliza vita. Amesema Iran imeshaonyesha utayari wake wa kufanya mazungumzo na sasa inasubiri Marekani kuonyesha utashi wa kisiasa na kuzingatia wajibu wake wa kimataifa katika maneno na vitendo. Amiri wa Qatar amethibitisha utayari wa Doha kuendelea na jukumu lake la upatanishi, akiahidi kutoacha juhudi zozote kusaidia amani, usalama, na utulivu wa eneo hilo.
Katika mazungumzo na Sultan wa Oman, Haitham bin Tariq Al Said, Rais Pezeshkian amesifu juhudi za kidiplomasia za Oman katika kuimarisha utulivu wa kikanda, akisisitiza hitaji la kubadilisha umoja wa kiibada wa ulimwengu wa Kiislamu kuwa ushirikiano wa vitendo na endelevu.
Hatimaye, katika mazungumzo na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kukuza mahusiano ya nchi mbili na kuanzisha amani ya kikanda. Rais Pezeshkian amebainisha shukrani zake kwa msimamo wa kimsingi wa serikali na wananchi wa Uturuki katika kuiunga mkono Iran dhidi ya uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na Israel, akisema kuwa jukumu la Uturuki katika kuendeleza michakato ya kidiplomasia ni la thamani kubwa.

4354620