IQNA

Iran yasema ushirikiano na mazungumzo ni njia bora ya kutatua matatizo

17:13 - April 14, 2012
Habari ID: 2304249
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, Tehran inaamini kwamba, ushirikiano na mazungumzo ni njia mwafaka na amilifu kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi matatizo mbalimbali.
Ramin Mehmanparast ameashiria mazungumzo ya Iran na kundi la 5 + 1 yaliyoanza leo huko Istanbul Uturuki na kusema kwamba, moja ya sababu za kufeli kwa mazungumzo yaliyotangulia ni kwamba, nchi zilizofanya mazungumzo na Iran zilitanguliza mbele siasa za vitisho na mashinikizo. Amesema, madola hayo yalikuwa yakidhani kwamba, mashinikizo yasiyo ya kimantiki dhidi ya Iran yangeweza kubadilisha azma ya Tehran ya kustafidi na nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani. Ameongeza kuwa, mara hii Tehran inataraji kuuona upande wa pili ukiheshimu haki za wananchi wa taifa hili na kuacha kupendekeza mambo yasiyo ya kimantiki ikiwa ni pamoja na kuachana na siasa za kindumakuwili kuhusiana na kadhia ya nyuklia ya Iran.
Duru nyingine ya mazungumzo ya Iran na kundi la 5+1 imeanza muda mchache uliopita huko Istanbul Uturuki. Saeed Jalili Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa anaiwakilisha Iran katika mazungumzo hayo; huku kundi la 5+1 likiwakilishwa na Bi Catherine Ashton Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya.
Kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, Mkuu wa Timu ya Mazungumzo ya Iran amesisitiza kwamba, Tehran iko tayari kufanya mazungumzo yenye natija na yenye kuimarisha ushirikiano. Jalili amewaambia waandishi wa habari kwamba, Tehran ina matumaini kwamba, kundi la 5+1 litaingia katika duru hii ya mazungumzo likiwa na utendaji na mtazamo huo ili kuyafanya mazungumzo ya mara hii kuwa na natija maridhawa.

985073
captcha