Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC jana Jumapili alitoa taarifa akitaka mashirika ya kutetea haki za binadamu na Umoja wa Mataifa ziwatetee mateka wa Palestina wanaoteseka kwenye jela za kuogofya za utawala haramu wa Israel.
Ihsanoglu amesisitiza udharura wa kuachiliwa huru mateka wa Palestina na kuongeza kwamba utawala huo umekuwa ukiwafunga jela raia wa Palestina bila kuwafikisha mahakamani na pia watoto wadogo kwa sababu za kisiasa. Amesema hali hiyo inaibebesha jamii ya kimataifa jukumu kubwa la kufanya juhudi za kusimamisha jinai na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Waapalestina wasio na hatia.
Katibu Mkuu wa OIC amebainisha wasiwasi wake mkubwa kuhusiana na hali mbaya inayowakabili wafungwa na mateka wa Palestina katika jela za utawala wa Israel na kuyataka mashirika ya kimataifa kufanya juhudi za kuachiliwa huru wafungwa hao mara moja.
Kwa wiki mbili sasa, wafungwa wapatao 1500 wa Kipalestina wamekuwa wakisusia chakula kulalamikia hali mbaya na mateso wanayopata katika jela za utawala huo. 996360