Sherehe za kutoa shukrani na kuwapongeza wanaharakati wa masuala ya Qur'ani ambazo zimedhaminiwa na Idara ya Masuala ya Qur'ani iliyo chini ya Wizara ya Sheria, Masuala ya Kiislamu na Wakfu ya Bahrain zimefanyika katika Msikiti wa Ijumaa wa Kituo cha Kiislamu cha Ahmad al-Fatih. Kwa mujibu wa gazeti la al-Wasat linalochapishwa Bahrain, sherehe hizo zimesimamiwa na Khalid bin Aal Khalifa, Waziri wa Sheria, Masuala ya Kiislamu na Wakfu wa nchi hiyo.
Akizungumza katika sherehe hizo, Farid Ya'qub Miftah, mwakilishi wa wizara iliyotajwa amesema kwamba taasisi na walimu wa Qur'ani Tukufu nchini humo wamefanya shughuli nyingi za kuvutia kwa ajili ya kunyanyua mafundisho ya kitabu hicho kitakatifu katika jamii ya Bahrain.
Wakati huohuo Aiman Abdul Ghani, mmoja wa wasimamizi wa vituo vya Qur'ani nchini Bahrain amewataka walimu wote wa Qur'ani na wanaharakati wanaoeneza mafundisho ya kitabu hicho katika jamii kufanya juhudi maradufu kwa madhumuni ya kueneza utamaduni wa Qur'ani nchini.
Mwishoni mwa sherehe hizo taasisi na vituo vya Qur'ani vilivyofanya vizuri katika kueneza mafundisho ya Qur'ani mwaka uliopita vilishukuriwa na kutunukiwa zawadi. 1041079