IQNA

Kiongozi Muadhamu: NAM inapaswa kushughulikia suala la Syria

23:32 - August 31, 2012
Habari ID: 2402224
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Jumuiya ya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM inapaswa kufanya ubunifu na kuhitimisha hali ya sasa inayotawala huko nchini Syria.
Ayatulllah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo katika mazungumzo yake na Nuri al-Maliki Waziri Mkuu wa Iraq na kubainisha kwamba, Iran ikiwa mwenyekiti wa NAM na Iraq ikiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zinaweza kutumia uwezo na nguvu za asasi hizo mbili na kuwa na taathira muhimu na sahihi katika masuala ya Mashariki ya Kati ikiwemo kadhia ya Syria. Aidha Kiongozi Muadhamu amekutana pia na Waziri Mkuu wa Syria na kusema kwamba, chanzo cha hali inayoshuhudiwa leo nchini Syria ni Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesisitiza kwamba, wasababishaji wakuu wa hali ya Syria ni watu wanaoyaunga mkono na kuyapatia silaha makundi yasiyowajibika nchini humo. Wakati huo huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutana na kufanya mazungumzo pia na Bi Sheikh Hasina Wajid, Waziri Mkuu wa Bangladesh na kusisitiza juu ya udharura wa kuweko ushirikiano wa nchi za Kiislamu na kutumia ipasavyo uwezo zilionao kwa ajili ya maslahi ya mataifa ya Kiislamu. Tahadhari ya Kiongozi Muadhamu kuhusu njama za maadui Wakati huo huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametahadharisha kuhusiana na njama hatari za maadui za kuzusha hitilafu za kikaumu na kidini katika nchi za Kiislamu. Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais wa Indonesia na kusisitiza juu ya udharura wa kutekelezwa malengo makuu ya kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM). Amesema kuwa, nchi wanachama wa jumuiya ya NAM ikiwemo Indonesia ambayo ni miongoni mwa waasisi wake, zinapaswa kushirikiana na kutumia uwezo wao na kuwa na taathira na mchango mkubwa katika masuala muhimu ya kieneo na kimataifa. Ayatullahil Udhma Ali Khamenei amesema, moja ya njama hatari kabisa za maadui ni kuzusha hitilafu na mapigano ya kimadhehebu hususan kati ya Waislamu wa madhehebu za Kishia na Kisuni. Ameongeza kuwa vitendo hivyo vinafanyika kwa uungaji mkono wa baadhi ya nchi kubwa za kibeberu na kwa kutumia vibaraka wao na mifano ya suala hilo inaonekana wazi katika nchi za Pakistan na Afghanistan. Kiongozi Muadhamu apongeza mapambano ya Waalgeria dhidi ya wakoloni Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo (Ijumaa) amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Algeria aliyeko hapa mjini Tehran na kupongeza hitoria ya kimapinduzi na jihadi ya wananchi wa Algeria dhidi ya wakoloni. Amesema kuwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran serikali ya Algeria daima imekuwa miongoni mwa washirika wazuri na inashiriki katika kambi ya kupambana na ubeberu. Amesisitiza kuwa Algeria inaweza kuwa na mchango muhimu katika Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) na kusema kuwa kuna nyanja nyingi za kupanua uhusiano wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni baina ya Iran na Algeria na kwamba mambo hayo yanapaswa kufanyiwa kazi. Wakati huo huo Spika wa Bunge la Algeria Abdul Qaid bin Saleh amesema mahudhurio makubwa ya viongozi wa nchi mbalimbali za dunia katika mkutano wa NAM mjini Tehran husuan katika kipindi cha sasa yana umuhimu mkubwa. Ameongeza kuwa Algiers inataka kupanuliwa zaidi uhusiano wake na Iran na kwamba suala hilo linapaswa kufuatiliwa kwa kuundwa kamisheni ya pamoja ya nchi hizo mbili. Ayatullah Khamenei: Kuna udharura wa kuwa macho mbele ya njama za wanaoyatakia mabaya mataifa ya Kiislamu Rais Omar al Bashir wa Sudan alikuwa miongoni mwa viongozi mbalimbali walioonana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei. Katika mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya udharura wa nchi za Kiislamu kufanya harakati kubwa zaidi katika masuala muhimu na kusisitiza kwamba Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) ni uwanja mzuri unaozipa nchi za Kiislamu na nchi zinazojitawala uwezo wa kuwa na taathira katika masuala mbalimbali ya kieneo likiwemo suala la Palestina na Syria. Amesisitiza juu ya udharura wa kuwa macho mbele ya njama za wanaoyatakia mabaya mataifa ya Kiislamu na akasema kuwa, tunapaswa kuwa macho na tusifanye makosa katika kutambua na kuchambua masuala mbalimbali. Katika mazungumzo hayo Rais Omar Hasan al Bashir wa Sudan ameeleza kufurahishwa na jinsi mkutano wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote ulivyofanyika kwa mafanikio hapa mjini Tehran na kusema kuwa, masuala ya Palestina na Syria ni miongoni mwa masuala muhimu na yanayotia wasiwasi. Amesisitiza pia juu ya ulazima wa kutumiwa uwezo wa jumuiya ya NAM kwa ajili y a kutatua masuala hayo.
1088470
captcha