Amesema kuwa juhudi zote za masuala ya kiutamaduni, sanaa na elimu zinapaswa kufanyika na kutekelezwa kwa ajili ya kustawisha zaidi ibada ya swala kati ya wananchi hususan kizazi cha vijana.
Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano huo ni hii ifuatayo:
Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu
Mwaka huu pia ninyi wanaume na wanawake mnaotafuta radhi zake Mwenyezi Mungu na hakika, mumepiga hatua nyingine katika njia ya kutekeleza wajibu wenu mkubwa wa Kiislamu, yaani kusimamisha na kudumisha swala kwa kuitisha mkutano huu. Ninawashukuru wahusika wote hususan Janabi Hujjatul Islam Bwana Muhsin Qaraati, mwanazuoni, mujahid, mkweli na mwenye imani thabiti ambaye ndiye nguzo kuu ya kazi hii kubwa, na namuomba Mwenyezi Mungu amlipe mema yeye na wenzake.
Pamoja na hayo yote tunapaswa kukiri kwamba, hadi sasa sisi viongozi wa mfumo wa Kiislamu bado hatujatekeleza wajibu wetu kikamilifu na ipasavyo katika uwanja huo.
Umuhimu wa swala unapaswa kueleweka vyema. Kauli inayosema: “Swala inapokubaliwa na Mwenyezi Mungu, kazi na huduma nyingine zote pia zitakubaliwa, na iwapo itakataliwa basi mambo mengine yote yatakataliwa,” inatudhihirishia hakika kubwa. Hakika hiyo ni hii kwamba, iwapo swala itawekwa katika nafasi yake inayostahiki katika jamii ya Kiislamu, basi juhudi zote nzuri za kimaada na kimaanawi zinashika njia yake kuelekea kwenye thamani aali na kuifikisha jamii katika kiwango kinachohitajika cha thamani za Uislamu; na iwapo tutaghafilika na umuhimu wa swala na ibada hiyo ikapuuzwa, basi njia hiyo haitakwenda sahihi na jitihada na juhudi zote hazitakuwa na taathira nzuri za kutufikisha katika kilele ambacho Uislamu umekiainisha kwa ajili ya jamii ya mwanadamu.
Uhakika huo unatutahadharisha na kutukumbusha wajibu mkubwa. Jitihada za kiutamaduni na za sanaa na mipango ya elimu na kadhalika vyote vinapaswa kupangwa na kutekelezwa kwa njia ambayo swala itaenea na kuimarika zaidi na kwa njia bora kati ya wananchi hususan vijana na mabarobaro, na watu wote wafaidike na chemchemi hiyo ya usafi na na inayong’arisha. Hapana shaka kuwa asasi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya mafunzo na utamaduni na vilevile Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) na mafisa wanaohusika na uendeshaji wa masuala ya misikiti wanapaswa kuhisi majukumu mazito zaidi kuliko watu wengine.
Mwombeni msaada Mwenyezi Mungu Mtukufu, mjifunge kibwebwe na muanzishe harakati mpya katika njia hiyo.
Mwenyezi Mungu awe auni na mlinzi wenu.
Sayyid Ali Khamenei
13/ Shahrivar/1391 (05/09/2012) 1092273