IQNA

Mtume avunjiwa tena heshima Ufaransa, Waislamu walaani kitendo hicho

14:57 - September 19, 2012
Habari ID: 2415338
Baraza la Waislamu wa Ufaransa (CFCM) limetoa taarifa likilaani vikali kukaririwa hujuma dhidi ya Uislamu nchini humo baada ya kuchapishwa tena vijikatuni vinavyomdhalilisha na kumtusi Nabii Muhammad (saw).
Vikatuni hivyo vimechapishwa katika jarida la kila wiki la Charlie Hebdo.
Gazeti la al Intiqad linalochapishwa Lebanon limeandika kuwa, Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu wa Ufaransa Muhammad Musawi amelaani vikali harakati hiyo ya kumdhalilisha Mtume wa Uislamu na amewataka Waislamu wa Ufaransa kuwa na subira.
Msimamizi wa Msikiti Mkuu wa Paris Dalil Bubakr pia amewataka Waislamu wa Ufaransa kulinda utulivu na akisisitiza kuwa anaelewa wasiwasi na maumivu yao yaliyosababishwa na kuchapishwa tena vijikatuni vinavyomvunjia heshima Mtume (saw) katika jarida la Charlie Hebdo, suala ambalo yumkini likazusha hasira kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Bubakr amesema kuwa inasikitisha kuwa nchini Ufaransa hakuna sheria ya kuwafikisha mahakamani watu wanaofanya vitendo vya kibaguzi na kuchochea chuki za kidini.
Jarida la kila wiki la Charlie Hebdo katika toleo lake la leo limechapisha tena vijikatuni vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) kwa kisingizio cha uhuru wa kusema na kuandika.
Ufaransa ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya.
Mwaka 2006 jarida hilo la Charlie Hebdo lilichapicha tena vijikatuni ambavyo awali vilichapishwa na gazeti la Jylllands Posten la Denmark, kitendo ambacho kilikabiliwa na hasira na malalamiko makubwa ya Waislamu kote duniani. 1102013


captcha