IQNA

Mchango wa Wanawake katika Hamasa ya Ashura

16:05 - November 25, 2012
Habari ID: 2453438
Ashura ni chemchemi ambayo daima ni yenye kutoa msukumo wa harakati baina ya vizazi vya mwanadamu.
Ashura ni chemchemi ambayo daima ni yenye kutoa msukumo wa harakati baina ya vizazi vya mwanadamu. Katika harakati adhimu ya Imam Hussein bin Ali AS mjukuu wa Mtukufu Mtume SAW, wanawake walikuwa na nafasi muhimu mno kutokana na kutambua wakati, masuuliya na majukumu na mambo hayo yanatajwa kuwa yalikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa katika kubakia na kuendelea kwa harakati iliyoanzishwa na Imam Hussein AS ya kusimama na kupambana na dhulma, madhalimu pamoja na upotoshaji dini.
Kuwa na mtazamo mpana na welewa wa dini ulioambatana na mapenzi aali kwa rudhia na Ahlul Bayt wa Mtume SAW ni miongoni mwa zilizokuwa sifa maalumu za wanawake waliokuwako katika harakati ya 'Ashura. Kwa hakika wao walifasiri na kutoa maana na fasili ya maneno kama huba, mapenzi, kujitolea, kusubiri, muqawama, na kusimama kidete katika kumlinda Imam Hussein.
Wanawake hao waliotengeneza historia, licha ya kuwa kama walivyo wanawake wengine uwepo wao ulikuwa umejaa, huba, huruma na mapenzi kwa ajili ya watoto na waume zao, lakini hawakuruhusu hisia zao ziwatale wakati wa kutetea dini na matukufu yake yaliyojidhihirisha na kujipamba katika harakati na mapambano ya Imam Hussein AS.
Kwa mtazamo wao ni kuwa, jukumu la Waislamu ni kuwa na welewa na muono wa mbali kuhusiana na dini sanjari na kuwa na ufahamu kuhusiana na maarifa ya Ahlul Bayt wa Mtume SAW na kuwa na urafiki nao, urafiki ambao unaambatana na huba na mapenzi kwao; kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika Sura ya Ash Shura aya ya 23:
Sema, siwaombi ujira isipokuwa mapenzi katika ndugu (yaani kwa kizazi changu).
Katika masiku ya mwisho ya maisha yake, Imam Hussein AS akiwa amezingirwa na maadui, alitumia fursa hiyo kuwatimizia hoja masahaba zake na kuwaambia kwamba, wanaweza kukhitari na kuchagua baina ya kuondoka katika medani ya vita na madhalimu na hivyo kusalimisha roho zao au kubakia na kuuawa. Imam alisema kuwahutu masahaba zake, "kila mtu ambaye amekuja hapa na ahli na famia yake, usiku huu huu anaweza kuichukua familia yake na kuipeleka sehemu yenye amani na usalama, kwani kesho watu watauawa na familia yangu itachukuliwa mateka."
Lakini wanawake waliokuwa katika medani hiyo, walisimama kidete tena bila kutetereka na kuwataka waume zao wawe bega kwa bega na Imam Hussein na Ahlul Bayt wa Mtume SAW.
*****
Tukio la Ashura ni tukio muhimu ambapo wanawake na wanaume kila mmoja yaani mwanamke na mwanaume alikuwa na nafasi na mchango wake. Uislamu unajifakharisha kwamba, kwa karne kadhaa hata kabla ya kujitokeza mapote mapya haya yanayodai kutetea haki za binadamu, dini hii tukufu ilikuwa imempatia mwanamke haki zake kwa mujibu wa fitra na maumbile yake.
Tukirejea katika historia ya Uislamu tunapata kwamba, Mtume SAW alifanya hima na idili kubwa kwa ajili ya kunyanyua kiwango cha ufahamu cha wanawake pamoja na utamaduni wao. Mtume SAW alikuwa akimleta mwalimu kwa ajili ya watu wa nyumbani kwake. Wakati mwingine baadhi ya wanawake walikuwa wakiambatana na binti yake vitani kwa ajili ya kuwatibu majeruhi wa vita. Aidha warithi wake yaani maimamu watoharifu, nao walifanya jitihada kubwa katika suala la malezi na mafunzo kwa wanawake na kwa hima na idili yao, jamii ikaondokea kupata wanawake wenye kujitolea, wa kupigiwa mfano na wasio na kifani. Matunda ya juhudi hizo tunaweza kuyashuhudia wazi na wadhiha baina ya wanawake waliokuwako katika msafara na kafila ya Imam Hussein AS katika ardhi ya Karbala.
Baadhi ya wanawake waliokuwako katika ardhi ya Karbala na katika tukio la Karbala ni watoto wa Imam Ali kama vile Zaynab, Ummu Kulthum, Fatima na Safia. Aidha walikuweko pia mabinti wa Imam Hussein As yaani Fatima, Sukaina, na Ruqaiyyah pamoja na mkewe Imam Hussein aliyejulikana kwa jina la Ummu Rubab na A'tikah mke wa Imam Hassan AS.
Bibi Zaynab AS binti mkubwa Imam Ali AS na dada yake Imam Hussein AS ni miongoni mwa majina ya wanawake yanayong'ara katika tukio la Ashura. Bi Zaynab ambaye amezikwa huko nchini Syria, alikuweko tangu mwanzoni mwa mwa harakati ya Imam Hussein pamoja na watoto wake wawili wa kiume. Katika usiku wa kuamkia Ashura, baada ya hali ya vita na kuuawa shahidi kueleweka kwa kila mtu na baada ya Bi Zaynab kushuhudia kwamba, masahaba wa Imam Hussein AS wanakwenda kumuona Imam hali ya kuwa wana shauku na hamasa kubwa iliyoambatana na furaha ya kusimama na kumtetea mjukuu wa Bwana Mtume SAW alifurahi mno. Aliondoka na kwenda kumuona kaka yake huyo hali ya kuwa ni mwenye tabasamu na bashasha kubwa.
Imam Hussein baada ya kumuona dada yake akiwa katika hali hiyo alisema, Dada yangu mpenzi, tangu tuondokea Madina, katu sijawahi kukuona ukiwa unatasamu namna hii, umepata khabari gani ambayo imekufurahisha kiasi hiki na kukufanya uonekane ni mwenye furaha namna hii? Bi Zaynab alimjibu Imam Hussein kwa kuashiria utiifu na himaya ya masahaba wa kaka yake. Imam Hussein baada ya kusikia maneno ya Bi Zaynab akasema, dada yangu mpenzi, tambua kwamba, masahaba ambao wako bega kwa bega na mimi ni marafiki na masahaba wangu. Babu yangu Mtume SAW aliniahidi kuhusiana na utiifu na urafiki wao kwangu."
*****
Historia inaonesha kuwa, baada ya tukio la kuhuzunisha na kutia simanzi la Karbala, Bi Zaynab AS alisimama kidete na kukabiliana barabara na dhulma za watawala madhalimu na majahili wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein AS. Kwa hakika maneno na muamala wa wanawake waliokuwa katika harakati ya Imam Hussein huko katika ardhi ya Karbala ni mambo ambayo mtu akiyatazama anaona ni kwa kiasi gani wanawake hawa walikuwa watiifu, waliokuwa na moyo wa subira na walijitolea na kuonyesha ushujaa wa hali ya juu wa kuvumilia taabu na masaibu. Wanawake hao licha ya kukabiliwa na masaibu na kushuhudia kwa macho yao mauaji ya kinyama kabisa yaliyofanywa na jeshi la batili la Yazid bin Muawiya, walisimama kidete na kutotetereka katika kumtetea mjukuu wa Mtume SAW Imam Hussein bin Ali AS.
Bibi Zaynab AS binti wa Imam Ali bin Abi Talib alionesha adhama kubwa katika harakati ya Karbala. Adhama ya bibi mwema huyo na yale yaliyonukuliwa kumhusu kuhusiana na msimamo wake thabiti katika mapambano ya Karbala ni jambo linaloonesha adhama na kusimama kidete bibi huyu katika njia ya haki. Kwa hakika subira ya Bibi Zaynab AS katika tukio la Karbala haina mithili. Ikiwa imepita nusu siku tu tangu kaka yake, mtoto wa kaka yake na watoto wake wawili wauawe shahidi mbele ya macho yake katika uwanja wa Karbala, alisimama kando ya kiwiwili cha kaka yake yaani Imam Hussein na akiwa na moyo thabiti na irada kamili alimtaka Mwenyezi Mungu apokee udh'hiya huo wa dhuria ya Bwana Mtume SAW.

السلام علی الحسين
و علی علی بن الحسين
و علی اولاد الحسين
و علی اصحاب الحسين
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh
captcha