IQNA

Al-Azhar yawaenzi dada watatu Wamisri waliohifadhi Qur'ani

11:29 - December 12, 2025
Habari ID: 3481651
IQNA-Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar katika mkoa wa Aswan, Misri, kimewatunuku zawadi na heshima maalumu dada watatu Wamisri waliokamilisha kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu.

Katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa na wanazuoni wa Al-Azhar na familia za eneo hilo, dada hao walipongezwa kama mfano bora kwa jamii, wakidhihirisha bidii, subira na mapenzi ya dhati kwa Qur'ani Tukufu, kama ilivyoripotiwa na gazeti la Al-Watan. Husna Salah Abu Zaid, mmoja wa dada hao na mwanafunzi wa miaka 19 katika Chuo cha Usul al-Din, alisema kuwa kuhifadhi Qur'ani lilikuwa ndoto yake tangu utotoni, na familia yake ilimsaidia hatua kwa hatua.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo yametimia kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na kwa msaada wa baba yao pamoja na walimu waliowalea kwa subira na malezi sahihi.

Dada yake, Alia Salah, mwenye umri wa miaka 24 na mhitimu wa Chuo cha Sheria ya Kiislamu, alisema kuwa masomo ya elimu za dini yalimsaidia kuielewa Qur'ani kwa undani zaidi, akimshukuru Mungu kwa kuwaweka yeye na dada zake katika njia moja ya kheri.

 Alishukuru pia familia yao kwa kuifanya nyumba yao kuwa “Nyumba ya Qur'ani,” na akawataja walimu wa utotoni na wa Al-Azhar kuwa ni vielelezo vya elimu na maadili. Rawda Salah, dada wa tatu mwenye umri wa miaka 22, alisema kuwa Qur'ani imebadili maisha yake na kumpa utulivu wa kipekee, akisisitiza kuwa familia yao iliwaunga mkono katika kila hatua.

Aliwahimiza Waislamu kuielewa Qur'ani na kutoiweka pembeni, akiomba Mwenyezi Mungu aijaalie Qur'ani kuwa mwombezi wao Siku ya Kiyama. Wazazi wa dada hao walisema siri ya mafanikio ya binti zao ni nidhamu ya kila siku, muraja’a ya mara kwa mara, na kukuza mapenzi ya Qur'ani ndani ya nyumba, huku wakisifu mazingira bora ya kielimu yaliyotolewa na Kituo cha Al-Azhar cha Aswan.

4322109

Habari zinazohusiana
captcha