
Mashindano hayo, yaliyopewa jina “Mashindano ya Kimataifa ya Albasira ya Kuhifadhi Qur’ani kwa Wenye Ulemavu wa Macho" yaliandaliwa jijini Jakarta wiki iliyopita na Jumuiya ya Kiislamu ya Dunia (MWL).
Wahifadhi wa Qur’ani wenye ulemavu wa macho kutoka nchi mbalimbali walishiriki katika mashindano hayo, na hafla ya kufunga ilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa MWL na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu, Sheikh Mohammed bin Abdulkarim Al-Issa; Spika wa Bunge la Indonesia Ahmad Muzani; na Waziri wa Masuala ya Kidini wa Indonesia Nasaruddin Umar.
Malengo ya tukio hili la Qur’ani yalikuwa kuunda roho ya mashindano miongoni mwa wahifadhi wa Qur’ani wenye ulemavu wa macho, kuwahimiza na pia kuheshimu kundi hili la wahudumu wa Qur’ani, kuonyesha nafasi ya wenye ulemavu wa macho (vipofu) katika jamii, kuimarisha uwezo wao wa hifdh na tilawa, na kuongeza imani yao kwa uwezo wao.
Mashindano yalifanyika katika makundi mbalimbali: kuhifadhi Qur’ani nzima pamoja na Matan al-Jazariyyah, kuhifadhi Qur’ani nzima (wavulana), kuhifadhi Qur’ani nzima (wasichana), kuhifadhi Juzuu 20 za Qur’ani, na kuhifadhi Juzuu 10.
Mshindi wa juu katika kundi la kuhifadhi Qur’ani nzima kwa wasichana alikuwa Zahra Khalili Samarin, mhifadhi wa Qur’ani mwenye ulemavu wa macho kutoka Iran.
Wakati wa mashindano haya, nakalah 300 za Qur’ani ya kielektroniki kwa mfumo wa nukta nundu (Braille) – teknolojia bunifu kwa ajili ya kuwahudumia wenye ulemavu wa macho duniani – zilisambazwa kwa washiriki.
3495683