IQNA

Istighfar katika Qur’ani Tukufu/ 6

Nafasi ya Istighfar katika kusamehewa dhambi na kuokolewa na moto wa jahannam

16:47 - December 23, 2025
Habari ID: 3481707
IQNA-Istighfar, yaani kuomba msamaha kwa Allah, ni ibada yenye athari nyingi katika maisha ya Mwislamu. Lengo kuu na la moja kwa moja la mwenye kuomba msamaha ni kusamehewa dhambi zake na kupata radhi za Allah.

Qur’ani Tukufu inasisitiza mara kwa mara kuwa msamaha wa dhambi ni njia ya kuokolewa na moto wa Jahannam na kufanikisha furaha ya milele. Aya ya 185 ya Surah Al Imran inasema: “Yeyote atakayeondolewa motoni na kuingizwa peponi, hakika amefuzu.”

Katika Surah Al Imran, Aya ya 133 inawaalika waumini kukimbilia msamaha wa Mola wao na Pepo isiyo na kikomo. "Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu."  Aya inayofuata (134) inabainisha matendo mema yanayosaidia kusamehewa dhambi: kutoa mali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu katika hali ya faraja na dhiki, kujizuia hasira, na kuwasamehe watu. Mwenyezi Mungu anasema: “Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.”

Aya ya 135 inaonyesha masharti ya istighfar yenye athari katika msamaha wa dhambi: “Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao - na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Mwenyezi Mungu? - na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua.”

Hii inaonyesha kuwa istighfar si maneno ya midomo pekee, bali ni tendo la moyo na matendo ya kujiepusha na kurudia makosa.

Aya ya 136 inahitimisha kwa kutaja malipo mawili makuu: msamaha wa dhambi na bustani za milele zenye mito inayotiririka. “Hao malipo yao ni msamaha kwa Mola wao Mlezi, na Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu, na mwema mno ujira wa watendao.”

Kwa hivyo, istighfar ni kitendo cha kiroho na kiutendaji kinachojumuisha kukumbuka Allah, kutubu kwa dhati, kujiepusha na kurudia makosa, na kuimarisha tabia njema kama kutoa sadaka, kujizuia hasira, na kuwasamehe watu. Hii ndiyo njia ya kusamehewa dhambi na kuokolewa na moto wa Jahannam, na hatimaye kupata Pepo ya milele.

3495276

Kishikizo: MAWAIDHA qurani tukufu
captcha