Katika ujumbe aliouandika kwa Kiarabu kwenye mitandao ya kijamii, Hujjatul Islam Qomi alisema: “Amani na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya watu wa Yemen, wenye subira na msimamo, waliobaki imara katika imani zao na kuonyesha urithi wa Kiislamu kwa Waislamu wote. Qur’ani Tukufu ni mlinzi na msaidizi wenu. Historia yenu mmeiunganisha na heshima na fahari. Kwenu Qur’ani si kitabu tu, bali ni damu inayotiririka katika mishipa ya upinzani.”
Wiki iliyopita huko Plano, Texas, Jake Lang, mgombea wa Seneti kutoka chama cha tawala cha Rais Trump cha Republican, aliivunjia heshima Qur’ani Tukufu hadharani, kitendo kilichozua hasira na kulaaniwa na Waislamu, wanaharakati wa haki za binadamu na waangalizi wa kimataifa. Tukio hilo liliibua ghadhabu kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Siku ya Ijumaa makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen walimiminika katika barabara na mitaa ya Sa’ada kushiriki maandamano ya kulaani kitendo cha kunajisiwa Qur'ani Tukufu nchini Marekani, sanjari na kupaza sauti zao kuiunga mkono Palestina, huku hasira zikiongezeka katika ulimwengu wa Kiislamu kutokana na wimbi la vitendo vya hivi karibuni vilivyo dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Maandamano hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu, "uhamasishaji wa jumla na utayari wa kuunga mkono Qurani takatifu na Palestina," kulingana na Al-Masirah ya Yemen. Mikutano kama hiyo pia imefanyika katika miji mingine kadhaa ya Yemen katika siku mbili zilizopita.
Washiriki wa maandamano nchini Yemen walinyanyua nakala za Qurani na mabango yanayoonyesha msimamo usioyumba kuelekea kitabu kitakatifu cha Uislamu. Waandamanaji hao wamesisitiza kwamba, "tusi lolote kwa Qurani Tukufu linamaanisha shambulio kwa Ummah mzima [wa Kiislamu]."
Waandamanaji pia walithibitisha tena mshikamano wao na Palestina, wakisema Yemen itaendelea kushiriki katika masuala makuu ya Ummah wa Kiislamu.
Kauli za viongozi wa Yemen
Jumanne iliyopita, Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah nchini Yemen alilaani vikali kitendo hicho cha kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu kilichofanywa na mwanasiasa wa Marekani huku akiwataka Waislamu kote duniani kusimama imara kulinda matukufu yao.
Maulamaa na wanazuoni wa Yemen wamelaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Marekani. Tukio la hivi karibuni la uhalifu huo limefanywa na mgombea mmoja wa Baraza la Seneti la Marekani.
Taha al-Hadri, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Yemen, amemwambia mwandishi wa televisheni ya Al-Alam pambizoni mwa mkutano wa maulamaa wa Yemen waliolaani kutovukiwa adabu Qur'ani Tukufu nchini Marekani, kwamba: "Mkutano huu si mkutano wa kawaida, bali umeitishwa ili kuakisi hisia za watu, uongozi wa Yemen, kambi ya Muqawama na hisia za watu huru duniani ambao wote kwa kauli moja wanapinga kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu sambamba na jinai za utawala wa Kizayuni huko Palestina.
Kwa upande wake, Sheikh Saeed Salameh, mmoja wa wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri, pia amesema: "Waislamu wa madhehebu yote ya Kisunni na Kishia, Mashafi'i, Maliki, Mahanafi na Mahambal, wote wanakubaliana kuhusu utakatifu wa Qur'ani Tukufu, Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambacho hakina chembe ya shaka ndani yake. Hatupendi udini na hatutaki watu wawe washupavu, lakini kama tutaacha vitendo viovu kama hivi vya kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu viendelee, basi hakuna mipaka itakayowekwa na maadui kuhusu matukufu ya dini yetu na mwisho tutashindwa kupata pa kushikilia.
Taarifa ya mwisho ya mkutano wa maulamaa na wanazuoni hao imetilia mkazo wajibu wa kujiimarisha zaidi Waislamu kwa ajili ya Jihadi, wakibainisha kuwa, vita vya leo ni vita vya ufahamu, ni vita vya welewa na ni vita vya dini na imani. Wamesema, wasomi ndio msingi wa kutetea heshima ya taifa na maadili yake matakatifu.
Kabla ya hapo, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani kwa maneno makali uhalifu na kitendo kiovu kilichofanywa na Mmarekani cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu, ikielezea tukio hilo kuwa la kichochezi linalotoa harufu mbaya ya chuki, na shambulio la wazi dhidi ya matakatifu zaidi ya Waislamu na maadili ya kidini na ya kibinadamu yanayowakilishwa na dini zote za mbinguni.
4324152