IQNA

Mwandishi Mkristo: Bibi Zahra (SA) Ni Kielelezo Kamili cha Fadhila

16:35 - December 13, 2025
Habari ID: 3481655
IQNA – Mwandishi Mkristo kutoka Lebanon amemwelezea Bibi Fatima Zahra (SA) kuwa kielelezo kamili cha fadhila, akisema kuwa yeye ndiye nguzo ya imani na heshima ya mwanamke.

Michel Kaadi, msomi na mwandishi Mkristo wa Lebanon, katika sehemu ya kitabu chake “Zahra, Kiongozi wa Wanawake wa Fasihi”, anaandika:

Kwa kuzaliwa kwa Zahra (SA), bintiye Mtume Muhammad (SAW),  mfumo wa upendeleo wa wanaume na desturi ya kuwazika mabinti wakiwa hai ulifikia kikomo. Harakati ya Zahra (SA) ya kuwakomboa wanawake kutoka katika dhulma ilifungua milango ya uhuru wa mwanamke. Wanawake Waarabu walitambua kutoka kwake sifa tukufu kama subira, ujasiri, ushujaa, elimu, uchaji, fadhila na maadili ya juu. Mtakatifu huyo aliweza kuwaweka wanawake katika nafasi za heshima na uwezo sawa na wanaume.

Kwa haiba yake iliyojaa heshima, Bibi Zahra (SA) hakukubali dhulma wala udhalilishaji. Badala yake, alibeba jukumu na mzigo mzito wa ujumbe wa kimungu na sheria za Uislamu, na akawa kioo cha imani na hadhi ya mwanamke.

Yeye ndiye ambaye malaika wa rehema walishuka kuzungumza naye; kwa sababu hiyo akaitwa Umm Abiha, “mama wa baba yake”, kabla hata ya kuwa mama wa nyota za Uimamu. Kizazi kutoharifu cha Mtume Muhammad (SAW) kilianzia kwake, na alikuwa ngome ya kulinda dini ya Uislamu na siasa ya haki.

Si ajabu basi kwamba Mtume (SAW) alimwita Fatima Umm Abiha. Na aya hizi za Qur’ani Tukufu zinathibitisha kuwa Mtume (SAW) haneni kwa matamanio yake: “Mwenza wenu hakupotea wala hakukosea. Wala haneni kwa matamanio yake. Hayakuwa ila ni wahyi unaofunuliwa kwake.” (An-Najm: 2–4)

Katika muktadha huu, Bibi Zahra (SA) ni kielelezo kwa wanawake na wanaume, mwalimu wa kwanza wa kike, na msimulizi wa mwanzo wa hekima.

Bibi Zahra (SA) aliwafundisha wanawake kulinda heshima na staha zao, na kuwakataza kuangukia katika matamanio ya ubadhirifu na kujipamba kupita kiasi kunakosababisha kuporomoka kwa maadili. Kwake, hijabu ilikuwa kama upanga dhidi ya uasi na maovu.

Kwa Mtume Mtukufu (SAW), hijabu humpa mwanamke uhuru wa ndani na hadhi ya kiroho, na huenda hili ndilo linalowasukuma watawa wa Kikristo kufunika nywele zao. Hijabu ni alama ya usafi, ulinzi, maadili na mwongozo.

Si jambo la kushangaza kusema kwamba leo, kwa baraka ya nafasi na utukufu wa Bibi Zahra (SA), mwanamke Mwislamu ni kinara wa maadili duniani.

Wakati ujumbe wa kinabii ulimshukia Mtume (SAW), athari zake zilionekana kwa waumini wa kiume na wa kike. Miongoni mwa wanaume, tunamtaja Imam Ali (AS), aliyebeba Qur’ani moyoni, nafsi na akili yake; na miongoni mwa wanawake, tunamtaja Fatima Zahra (SA).

Kwa Ali (AS), uwezo wa ufahamu ulitimilika kwa nguvu ya Mwenyezi Mungu; na kwa Zahra (SA), ujumbe huo ulifikia kilele chake, kiasi kwamba tunaweza kusema bila shaka kuwa yeye ni muujiza.

Ikiwa Imam Ali (AS) ni muujiza wa Mtume (SAW), nuru ya Uislamu na mwalimu wa Qur’ani Tukufu, basi Bibi Zahra (SA) ndiye shahidi bora wa ukweli huo. Jabir bin Abdullah Al-Ansari ananukuu hadithi ya kimungu: “Ewe Ahmad, lau si Ali nisingekuumba, na lau si Fatima nisingewaumba nyote wawili…”

Zahra (SA), kwa fadhila zake ambazo hakuwahi kuziacha hata kwa muda mfupi, anasimama mbele ya umma huu kama mama wa baba yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na hilo si jambo la kushangaza, kwani anatoka katika nyumba ya Mtume (SAW) iliyotumwa kuondoa ujinga na ukabila.

Fatima, mwanamke mtakatifu, alikuwa rafiki na mfariji wa baba yake tangu utotoni. Maoni yake yalikuwa karibu na ya Mtume, na katika nyakati za dhiki, alipokuwa akidhuriwa na maadui wa ujumbe, yeye ndiye aliyekuwa faraja yake. Mara nyingi alimfuta Mtume jasho usoni kwa vidole vyake, na alisimama imara katika misimamo yake. Maadamu alikuwa hai, alitetea nuru ya kimungu, maslahi ya umma na mustakabali wa Uislamu.

Yote haya yanaashiria ukubwa wa Fatima Zahra (SA), kama vile Qur’ani Tukufu inavyomrejea Maryam (SA), binti wa Imran, hata alipokuwa tumboni mwa mama yake miaka elfu mbili iliyopita. Aya zinazomhusu Maryam (SA), tafsiri na kiini chake, pia zinamhusu Zahra (SA), kiasi kwamba watu wamemchukulia kuwa kipimo cha fadhila na sifa tukufu.

captcha