IQNA

Kiongozi wa Ansarullah alaani ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wanawake wa Palestina

11:17 - December 12, 2025
Habari ID: 3481649
IQNA-Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah nchini Yemen, Abdul‑Malik al‑Houthi, amelaani vikali ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wanawake wa Palestina, akisema maelfu ya wanawake—akiwemo wajawazito, wasichana wadogo na wazee—wameuawa katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu.

Akizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Bibi Fatimah Zahra (SA), binti mpenzi wa Mtume Muhammad (SAW), al‑Houthi alionya kuwa Ummah wa Kiislamu kwa sasa unakabiliwa na moja ya vita hatari zaidi vya upotoshaji wa fikra, vinavyolenga kuwafanya watu watengane na misingi ya imani yao.

Alisema vita hivi vya kisaikolojia vinakuza tamaduni na mitazamo inayowapotosha Waislamu kutoka njia ya Uislamu wa kweli na kuwaelekeza katika mkondo wa wale waliopotea na wanaostahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.

Kiongozi huyo wa Ansarullah alibainisha kuwa madhara ya vita laini yamekuwa makubwa kuliko yale ya kijeshi, na ndiyo chanzo cha mkanganyiko, mgawanyiko, udhalilishaji na utegemezi uliopitiliza wa mataifa ya Kiislamu kwa serikali za Magharibi.

Aliongeza kuwa maadui wamezitawala serikali nyingi za Kiislamu, wakachukua rasilimali za mataifa ya Waislamu, kujenga kambi za kijeshi katika ardhi zao, na kutumia nguvu kazi ya Waislamu kwa maslahi yao binafsi.

Kwa mujibu wake, maadui pia wameporomosha hadhi ya kibinadamu, maadili na roho ya Kiislamu miongoni mwa Waislamu, jambo linaloonekana wazi katika misimamo dhaifu kuhusu mauaji ya halaiki ya Wapalestina.

Al‑Houthi aliikosoa vikali dunia ya Kiarabu na Kiislamu kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti, akisema baadhi ya tawala za Kiarabu zimefikia hatua ya kutoa msaada wa kifedha, kijasusi na kimataifa kwa utawala wa Kizayuni huku zikiwazuia wananchi wao kuchukua hatua yoyote ya maana kwa ajili ya Palestina.

Alionya kuwa Ummah wa Kiislamu unakabiliwa na msukosuko mkubwa wa kuporomoka kwa uelewa, maadili na thamani za msingi. Alisema adui wa Kizayuni sasa amefikia kiwango cha kutaka kuhalalisha uvamizi wa kila namna dhidi ya Waislamu, ikihusisha riziki zao, heshima, ardhi, maeneo matukufu na imani yao. Aidha, aliwatuhumu wanafiki kwa kukubali utawala kamili wa adui huyo katika eneo la Asia Magharibi na kujipanga upande wake, wakisaliti dini, heshima, uhuru na utu wao kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, al‑Houthi aliikosoa serikali ya  kundi la HTS nchini Syria, akiitaja kuwa ya kinafiki, inayoshirikiana na Marekani na kutumikia maslahi ya Israel. 

Alisema miongoni mwa dalili za wazi za uhalifu wa utawala wa Kizayuni ni kuendelea kukiuka makubaliano ya kimataifa, ikiwemo makubaliano ya kusitisha mapigano Lebanon na Gaza.

Alisisitiza kuwa Ummah wa Kiislamu unapaswa kujifunza kutoka kwa mifano bora ya Kiislamu, wanaume na wanawake wa uchaji, uelewa na athari njema, ili kurejesha hadhi yao ya kibinadamu, fahari ya kiimani na nafasi yao duniani. Al‑Houthi alihitimisha kwa kusisitiza kuwa Waislamu wanapaswa kutekeleza wajibu wao wa kusimamisha uadilifu, kuwatetea wanyonge na kukabiliana na madhalimu, badala ya kubaki tegemezi na wanyonge mbele ya nguvu za kiburi.

3495699

Habari zinazohusiana
captcha