IQNA

Msomi wa Algeria

Hoja za Qur'ani za Bibi Fatima Zahra (SA) ni kielelezo kwa Waislamu wote

11:37 - December 12, 2025
Habari ID: 3481652
IQNA-Profesa mmoja wa chuo kikuu kutoka Algeria amesema kuwa hoja za Qur'ani Tukufu alizotumia Bibi Fatimah Zahra (SA) katika kutetea misingi ya haki na uadilifu ni kielelezo cha vitendo ambacho Waislamu wote wanapaswa kukifuata.

Akizungumza na IQNA katika maadhimisho ya kuzaliwa kwa Bibi Zahra (SA), Bintiye Mtume Muhammad (SAW), Profesa Sadiq Saliymiyyah alisema kuwa Bibi Zahra (SA) alisimama imara akitumia Qur'ani kudai haki yake ya kurithi kutoka kwa baba yake.

Aliongeza kuwa katika tukio la Saqifa, Bibi Zahra (SA) aliwafundisha Waislamu namna ya kujadiliana kwa hoja za Qur'ani, kusimama kidete katika misingi ya haki, na pia kuwa mfano bora kwa wanawake katika familia zao. Akitaja fadhila na hadhi ya Bibi Zahra (SA), alisema kuwa yeye ndiye mwanamke bora zaidi katika historia yote, mwenye sifa kamilifu za kimaadili na kitabia.

Alisisitiza kuwa Qur'ani Tukufu na Ahlul-Bayt (AS) ni kitu kimoja, na kwamba Bibi Zahra (SA) ni taswira hai ya “Qur'ani inayonena,” na watoto wake pia wako katika daraja hilo. Kuhusu nafasi yake katika uwanja wa kijamii, Profesa Saliymiyyah alisema Bibi Zahra (SA) alikuwa mfano wa uthabiti, ukweli na msimamo usiotetereka. Alikumbusha kuwa katika suala la ardhi ya Fadak, Bibi Zahra (SA) aliwajibu waliopora haki yake kwa hoja za Qur'ani dhidi ya hadithi iliyotungwa. Akirejea tukio la Saqifa, alisema miongoni mwa aya alizowasomea Ansar ni aya ya 13 ya Surah At-Tawbah, inayowataja wanaovunja ahadi, wanaotaka kumfukuza Mtume (SAW) na wanaoanzisha vita kuwa ni viongozi wa kufri wanaopaswa kupingwa.

Bibi Zahra (SA) aliwalinganisha watu hao na viongozi wa Saqifa, akawauliza Ansar kwa nini walinyamaza na kujiunga nao. Profesa Saliymiyyah alisema Bibi Zahra (SA) aliwafundisha Waislamu namna ya kutumia Qur'ani katika hoja na namna ya kusimama katika misingi ya haki, na akawafundisha wanawake wa Kiislamu kuwa nguzo na mifano bora kwa familia na watoto wao. 

 4319574

captcha