
Akizungumza na Mwambata wa Utamaduni wa Iran nchini Uganda, Bw. Abdollah Abbasi, Sheikh Mubajje alisifu shughuli nyingi za kidini na kitamaduni zilizotekelezwa na Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini humo.
Alitaja kwa heshima mkutano wa kielimu uliolenga mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo, vipindi zaidi ya 130 vya kila wiki vinavyojulikana kama “Mtazamo Kuhusu Amani” kupitia Redio ya Kiislamu ya Bilal, pamoja na mashindano ya Qur’ani Tukufu yaliyofanyika kitaifa mara kadhaa. Sheikh Mubajje pia alimshukuru afisa huyo wa utamaduni wa Iran kwa kumualika Kwenda Tehran kushiriki Maonyesho ya 32 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu na vikao maalumu vya kielimu.
Aidha, Mufti Mkuu ametoa shukrani zake za dhati kwa msaada wa Iran kwa watu wa Gaza wanaodhulumiwa, na akalaani tena uvamizi wa kijeshi uliofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran mnamo mwezi Juni. Amemuomba Allah SWT aijaalie Iran iweze kuwa na amani, usalama, utulivu, mafanikio na heshima.
Mwanzoni mwa kikao hicho, Bw. Abbasi, ambaye muda wake wa utumishi unakaribia kukamilika, aliwasilisha ripoti fupi ya shughuli za Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Uganda kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Alisisitiza mchango na ushirikiano wa Mufti Mkuu katika utekelezaji wa shughuli hizo.
Mwisho wa kikao, Sheikh Mubajje alikabidhi cheti cha shukrani na vitabu viwili kwa balozi huyo wa Iran, akitambua na kushukuru juhudi zake za thamani katika kipindi cha utumishi wake Uganda.
4324144