
Abdul Rahman, kijana mwenye umri wa miaka 20 aliyezaliwa kipofu, ameihifadhi Qur’ani Tukufu neno kwa neno, akijitolea kwa moyo wa dhati bila kutafuta zawadi wala sifa, bali akitafuta aya ya kujifunza na dua ya kusoma katika kila sajda. Ushindi wake umelitangaza jina lake katika duru za kimataifa na kuibua fahari kubwa kwa kijiji chake.
Katika hafla iliyofanyika katika Msikiti wa Nabii Isa (AS), wakazi wa Tabloha walimshangaza Abdul Rahman kwa kumpa zawadi ya gari, ishara ya heshima na mapenzi kwa juhudi zake za kiroho. Tukio hilo lilipokelewa kwa shangwe, makofi na furaha tele, likiwa ujumbe wazi kwamba anayebeba Qur’ani Tukufu moyoni, mioyo ya watu humbeba juu ya mabega yao.
Ibrahim al-Hamoudi, mkazi wa Tabloha, alisema kijiji kinajivunia mafanikio ya kijana wao kama ushindi wa kimataifa. Aidha, Abdul Rahman alipokea cheti cha heshima na kiasi cha paundi 10,000 za Kimasri kutoka hazina ya Waislamu wa kijiji na mwalimu wake, Mohamed al-Atwi. Gari hilo, lenye thamani ya takribani nusu milioni paundi, limetolewa na kijana mmoja bora wa Tabloha na linatarajiwa kukabidhiwa rasmi wiki ijayo.
Akizungumza kwa furaha, Abdul Rahman aliwashukuru watu na vijana wa kijiji chake kwa msaada wao wa kudumu tangu utotoni hadi safari yake ya kuhifadhi Qur’ani Tukufu, akisema msaada huo umemwezesha kuendeleza njia yake na kulinua jina la kijiji chake katika duru za kimataifa.
/3495810