
Watu walikusanyika nje ya msikiti wakiwa na brashi na rollers, wakifunika alama za misalaba ya Kikristo zilizochorwa ukutani kutoka upande mmoja wa jengo hadi mwingine. Kamera za usalama zilimnasa mwanaume mzungu anayeonekana kuwa na umri wa miaka 30 akifanya uharibifu huo tarehe 7 Desemba majira ya saa 3 usiku.
Imam wa msikiti huo, Hesham Sabbah, alisema Masjid Ash Shura limekuwa sehemu ya jamii tangu miaka ya 1980 na kwamba kwa muda mrefu hakukuwa na vitisho vyovyote, jambo lililowafanya waamini kuwa hali ya usalama ilikuwa imeimarika.
Polisi wa Norfolk wanaendelea na uchunguzi na wanataka umma kuwasaidia kumtambua mtu anayedhaniwa kuhusika.
Mwendesha mashtaka wa jimbo hilo, Ramin Fatehi, alisema bado haijabainika iwapo tukio hilo ni uhalifu wa chuki, ingawa uwezekano huo haujatupiliwa mbali, kwani uamuzi utategemea ushahidi utakaokusanywa.
Alifafanua kuwa kitendo kinacholenga kuwatisha watu kwa misingi ya rangi, dini, asili ya mababu, utaifa, jinsia au ulemavu kinaweza kutajwa kuwa uhalifu wa chuki.
Takwimu za FBI zinaonyesha kuwa kati ya 2021 na 2025, visa 20 vya uhalifu wa chuki viliripotiwa Norfolk, ambapo ubaguzi wa rangi ulikuwa sababu kuu, ukifuatiwa na dini. Hata hivyo, wataalamu wanasema takwimu hizo huenda hazioneshi ukubwa halisi wa uhalifu unaochochewa na chuki.
Mmoja wa wakazi, Noel Young, alisikia kuhusu tukio hilo kupitia makundi ya kijamii na alijitokeza kusaidia kupaka rangi tarehe 10 Desemba, akisema kuwa majirani wema hawawezi kukaa kimya wanapoona uovu.
Imam Sabbah alisisitiza kuwa msikiti hautatetereka kiroho kutokana na tukio hilo, akitoa nasaha kwamba “hatupigani moto kwa moto, bali tunapambana kwa maji — hiyo ndiyo hekima.” Kwa kuwa polisi wamezuiwa kutumia teknolojia ya utambuzi wa sura, wanategemea taarifa kutoka kwa wananchi ili kumtambua mhusika.
3495705