IQNA

Siri ya kudumu harakati ya Imam Hussein AS

16:32 - November 25, 2012
Habari ID: 2453440
Ashura ni tukio ambalo imepita miaka 1373 tokea kujiri kwake lakini si tu kuwa tukio hili la kihistoria linawavutia Waislamu bali pia wapenda uhuru kote duniani wamevutiwa na yaliyojiri katika jangwa la Karbala.
Katika kipindi chote cha historia, kumejiri matukio mengi ambayo akthari yamesahaulika. Lakini tukio la Karbala ni la aina yake kwani tokea kujiri kwake hadi sasa limekuwa likivutia hisia za wengi na kuleta nuru katika nyoyo zilizokuwa kizani.
Siku ya 10 ya mwezi Muharram mwaka 61 Hijria Qmaria, kilio cha Imam Hussein AS na wafuasi wake cha kutaka haki kimebakia na kudumu katika kurasa historia. Leo kilio cha Imam Hussein AS kimewafikia watu wenye kiu cha kusikia kilio cha haki. Tuko katika siku za kukumbuka kuuawa shahidi Mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS na wafuasi wake katika jangwa la Karbala.
Uislamu, umejengeka katika fitra na hii fitra inawatazama wanaadamu wote kuwa ni kitu kimoja. Ni kwa sababu hii ndio mwanaadmau katika maumbile yake ya dhati anamtafuta Mwenyezi Mungu, uadilifu, umaridadi , uhuru na maisha ya milele. Lakini baadhi ya wakati kutokana na kughafilika, madhambi au matukio ya kijamii, kiuchumi na kisiasa mwanadamu huondoka katika mkondo wa ujumbe wa fitra. Kwa hivyo jukumu kubwa zaidi la Mitume na viongozi wa kidini ni kuwatakasa wanadamu na kuwakumbusha kuhusu neema walizozisahau za Mwenyezi Mungu.
Kwa hivyo tunaweza kusema kuwa jukumu kuu la Imam Hussein AS lilikuwa ni kuwaongoza wanaadamu katika njia sahihi na maadili bora zaidi ambayo yanaenda sambamba na fitra.
Imam Hussein AS alitaka kuondoa vizingiti vilivyokuwepo katika kufikia malengo haya ya juu. Kizingiti kikubwa katika njia hii kilikuwa ni utawala wa kiimla wa Bani Umayya ambao haukuwa ukiwapa watu fursa ili waweze kuitikia wito wa fitra. Kwa hivyo katika zama za utawala wa Bani Umayya, watu walikuwa mbali na masuala ya kutafuta haki, kupigania uhuru pamoja na kueneza maadili mema na uadilifu. Kilichojiri wakati huo ni kuenea ufisadi na ukatili na watu kupoteza ubinaadamu wao pamoja na thamani za kidini.
Katika zama hizo, Imam Hussein AS alianzisha harakati na mapambano ya kuwarejesha watu katika mafundisho ya kidini na thamani za juu za kibinaadamu. Nukta hii inaashiria muelekeo wa kimataifa wa mapambano ya Imam Hussein AS kwani harakati yake iliwahusu wanadamu wote.
Yamkini ni kwa sababu hii ndio Mahatma Gandhi kiongozi wa ukombozi India alisema kuwa harakati ya Ashura ilikuwa ilhamu ya harakati na mapambano yake dhidi ya mkoloni Muingereza.
Waandishi wengi wanaotetea haki duniani kama Kurt Frischler wa Ujerumani wamezungumzia adhama ya moyo na shakhsia ya juu ya Imam Hussein AS. Na hii ni kwa sababu mapamabno ya Imam Hussein AS yalikuwa mwamko wa kurejea katika thamani asili za mwanadamu na hivyo wito huu umekuwa wa kudumu kwa wote.
Imam Hussein AS alianzisha mapambano yake ili kutenganisha baina ya haki na batili. Alifahamu kuwa nguvu za utawala wa Yazid ulikuwa umejengeka katika misingi ya batili na iwapo ungeendelea hivyo, basi kungeshuhudiwa kuangamia kazi zote za mitume za kueneza uadilifu na ukweli. Kwa hivyo katika vikao vyake tafauti mtukufu huyo alifafanua na kuweka wazi haki na batili.
Kwa mtazamo wa Imam Hussein AS, batili huwa na nguvu ya kidhahiri na kupuuza mipaka ya mwenyezi Mungu na kupelekea kujitokeza kwa muundo wa utawala wa kiimla kisha kuwachukua watu mateka hadi kiasi ya wao kushindwa kutetea haki zao.
Tokea kuumbwa Adam kulikuwepo mapambano baina ya haki na batili na vita vingi katika historia ya mwanaadamu vilijiri kwa ajili ya hayo mawili. Katika kipindi muhimu zaidi, Imam Hussein AS alijitokeza kama mbeba bendera ya haki alipokabiliana na Yazid ambaye alikuwa mbeba bendera ya batili. Ili kulinda haki na kuweka wazi njia yake hadi siku ya qiyama, Imam Hussein AS, familia yake pamoja na wafuasi wake watiifu; wote kwa pamoja walitoa maisha yao muhanga. Ashura ni kielelezo cha vita vya daima baina ya haki na batili na thamani bora dhidi ya upotofu.
Ni kwa msingi huu ndio maana kama ambavyo tukio la Ashura limebakia hai na kudumu katika historia na jamii mbalimbali na hivyo kuwalinda wanaomuabudu Mwenyezi Mungu, wapiganiao uhuru na wanapoinga dhulma pia watabakia hai na kudumu siku zote.
Moja ya sababu nyingine za kudumu harakati adhimu ya Karbala ni uwazi wa mwamko huo. Imam Hussein AS wakati akianzisha mapambano yake makubwa, awali kabisa alibainisha utambulisho wa mapinduzi yake kwa njia ya wazi kabisa. Aliwafahamisha watu kuwa mapamabano yake yalilenga kupinga dhulma na kuhuisha Uislamu sambamba na kuwaokoa watu kutoka katika shari ya utawala wa Yazid. Alibainisha hata mbinu za mapambano ambazo zilipaswa zitumike.
Kwa hivyo, katika mapamabano ya Karbala kila kitu kilikuwa wazi ili katika mustakabali asijitokeze mtu kumkosoa Imam au apotee katika kufuata njia yake.
Imam Hussein AS katika wosia wake kwa Muhammad Hanafiyya aliweka wazi utambulisho wa mapambano yake na kusema yamejengeka katika msingi wa Kiislamu. Alisema mapambano yake yalikuwa na lengo la kutekeleza sheria za Kiislamu na kuangamiza utawala fisadi wa Bani Umayya na kuanzisha utawala adilifu wa Kialawi.
Mtukufu huyo vilevile katika kubainisha mbinu alizotumia kufikia malengo ya mapambano yake, alisisitiza kuhusu kuamurisha mema na kukataza mabaya ili kurekebisha jamii na kuwaokoa watu kutoka katika dhulma na utawala wa kiimla ambao haukuwa ukizingatia uadilifu. Imam aidha aliwataka watu watekeleze sira ya Mtume SAW na Imam Ali AS.
Imam Hussein AS akizungumza Makka alisema: "Ewe Allah! Unajua kile ambacho tunakifanya katika jamii si kwa sababu ya kupata mamlaka na utawala na wala si kwa ajili ya kupata utajiri. Sisi tunataka kuonyesha njia ya dini yako, tufanye marekebisho katika miji yako, waja wako waliodhulumiwa waishi katika utulivu na usalama na waweze kukutii Wewe pasina bughudha. Sisi tumeazimia kutekeleza yaliyofaradhishwa katika Uislamu, Suna ya Mtume SAW na sheria za Allah."
Mtukufu huyo katika hotuba yake aliashiria mahitajio ya kimsingi kabisa ya wanadamu. Je, inawezekana mapinduzi yajiri kwa sababu ya kufikia malengo ya kimsingi zaidi ya jamii za wanadamu na yasidumu milele?
Nukta nyingine iliyopelekea mapambano ya Ashura yawe ya kipekee ni kuwa, mwamko huu ulikuwa mwamko wa kiakhlaqi.
Katika historia kumejiri mapinduzi mengi ambayo yalitoa mhanga akhalqi katika mkondo wa mapambano. Lakini katika mapambano ya Karbala, suala la akhlaqi na maadili bora lilikuwa mhimili mkuu. Kuhusu hili tunaweza kuashiria hapa muamala wa Imam Hussein AS na maadui. Katika mapambano ya Karbala, mtukufu huyo hakuchukua hatua yoyote inayopingana na maadili ya Kiislamu.
Wakati Imam Hussein AS alipowasili Nainawa, Hurr ibn Yazid Ar-Riyahi kamanda wa jeshi la adui alipomlazimisha mtukufu huyu kukaa Karbala, Zuhair bin al Qain kati ya masahaba zake ambaye alikuwa kamanda maarufu wa kijeshi alimpa pendekezo Imam Hussein AS kuwa kutokana na kuwa idadi ya maadui walikuwa wachache katika kipindi hicho na wengine bado hawajafika, basi waanzishe vita. Lakini Imam alisema: “Mimi nazingatia msingi wa kiakhlaqi ambao ni kuwa sitakuwa mwanzishaji vita. Sisi hatutaanzisha vita na hawa.” Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kuwa katika siku ya Ashura Hurr ibn Yazid Ar-Riyahi alitubu na Imam Hussein alikubali tauba yake.
Tukio la Ashura limejaa nukta nyingi ambazo zinaonyesha kuwa mapambano ya Karbala yalikuwa ya kiakhlaqi kabisa na yalifuata misingi ya kibinadamu na Kiislamu.
Ni kwa sababu hii ndio kila mtu awe Mwislamu au asiyekuwa Mwislamu anapoangalia mapambano ya Imam Hussein AS anayatazama mapambano hayo kwa mtazamo tafauti na kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na thamani za kiakhlaqi za harakati ya Imam Hussein AS. Hakuna shaka kuwa mapambano na harakati ya Imam Hussein AS ni ya kipekee katika historia ya Kiislamu na dunia na kama alivyosema Shahid Mutahhari shakhsia ya Imam Hussein ni ya kipekee kabisa.
Mwamko wa Imam Hussein ni kielelezo cha hali ya juu cha thamani za kiakhlaqi na kibinadamu. Hii ni kwa sababu katika medani ya vita wakati huo, mapambano yalikuwa baina ya imani na umaanawi kwa upande moja na upande mkabala ukafiri na ufisadi. Waliopigana upande wa haki hawakuwa na budi ila kuibua hamasa na ushujaa. Kwa hivyo mapambano yaliyojawa hekima na kwa wakati wake ya Imam Hussein yamebakia kama johari yenye thamani katika historia na ujumbe wake unaendelea kufikia kizazi hadi kizazi kingine.


captcha