IQNA

Rais Ahmadinejad atoa salamu za Krismasi na Mwaka Mpya

13:55 - December 27, 2012
Habari ID: 2471007
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za kheri na fanaka kwa viongozi Wakristo na mataifa yao kote duniani kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Nabii Issa AS na kuwadia mwaka mpya wa 2013 Miladia.
Katika ujumbe wake huo, Rais Ahmadinejad amesema anaamini kuwa, njia pekee ya kuinusuru dunia kutoka katika migogoro shadidi ya kimaadili, kijamii na kiutamaduni ni kurejea katika mafundisho matukufu ya Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu.
Aidha amesema kutoweka masuala ya kiroho na maadili bora kumemfanya mwanadmu wa leo apiganie haki zake halisi zikiwemo uadilifu na uhuru.
Rais Ahmadinejad pia amewatakia Wakristo mwaka uliojaa baraka na fanaka na kumuomba Mwenyezi Mungu azijaalie afya, mafanikio na ustawi serikali na mataifa ya Wakristo duniani.
Katika ujumbe wake huo wa Krismasi na Mwaka Mpya, Rais Ahmadinejad ameelezea matumaini yake kuwa, kwa juhudi za pamoja tutashuhudia kurejea utulivu na maisha bora kwa watu wote pamoja na kupatikana uadilfu endelevu kwa msingi wa tauhidi, maadili mema na upendo.
1160549
captcha