IQNA

Visa vya kuwavunjia heshima Mitume wa Mwenyezi Mungu vyaendelea katika filamu za Marekani

18:08 - February 23, 2013
Habari ID: 2501255
Makundi ya wanaharakati wanaopinga dini nchini Marekani ambayo yamekhitari sekta ya filamu kama wenzo wa kufikia malengo yao yameendeleza sera zao za kuwavunjia heshima Mitume wa Mwenyezi Mungu kwa kuanza kutangaza filamu mpya iliyopewa jina la "DJesus Uncrossed" (Masih Hakusulubiwa).
Tovuti ya CNBC imeripoti kuwa, matangazo ya filamu ya Kimarekani iliyopewa jina la "Masih Hakusulubiwa" ambayo inamvunjia heshima Nabii Issa bin Maryam (as) na kuoneshwa akiwa amebeba silaha katika vita vya kikatili na umwagaji damu, yamepingwa vikali na jamii ya Waislamu wa nchi hiyo.
Matangazo ya filamu hiyo yametolewa katika kipindi cha vichekecho kinachofuatiliwa na watu wengi cha Saturday Night Live katika kanali ya televisheni ya NBC ya Marekani na yamewachukiza mno mamilioni ya Waislamu na Wakristo kote duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Uhusiano wa Kiislamu na Marekani (CAIR) Nahad Awadh amesema kuwa kupotoshwa ujumbe wa amani wa Nabii Issa Masih (as) kwa njia hii kumewaumiza mno Wakristo, Waislamu na watu wote wanaoamini ujumbe wa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu.
Amesema filamu kama hiyo inayomvunjia heshima shakhsia mtakatifu na anayeheshimiwa na mabilioni ya Waislamu na Wakristo kote duniani haiwezi kukubaliwa.
Filamu ya Djesus Uncrossed inapotosha sura halisi ya Nabii Issa Masih (as) na kumdhihirisha Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu akiwa na silaha katika vita vya umwagaji damu na Warumi.
Hii si mara ya kwanza kwa Mitume wa Mwenyezi Mungu kuvunjiwa heshima katika filamu zinazotengenezwa Marekani. Mwaka jana filamu ya Kizayuni na Kimarekani iliyopewa jina la "Innocence of Muslims" inayomdhalilisha na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) ilioneshwa nchini Marekani na kukabiliwa na malalamiko ya Waislamu kote duniani. 1193484

captcha