IQNA

Imam Khamenei: Maadui wanachukia maendeleo ya wananchi wa Iran

11:09 - March 08, 2013
Habari ID: 2507876
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amevitaja vikwazo na kadhia ya nyuklia kuwa ni changamoto mbili zinazoukabili mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, pamoja na kuwepo changamoto hizo wananchi wa Iran bado wanapiga hatua mbele kimaendeleo na jambo hilo linawakera na kuwakasirisha mno maadui.
Akizungumza leo Alkhamisi na mkuu na wajumbe wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu linalomchagua Kiongozi Muadhamu, Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameelezea maendeleo makubwa ya wananchi wa Iran katika kipindi cha miaka 34 iliyopita na kuongeza kuwa, kadhia ya nyuklia ni moja kati ya changamoto zilizoukabili Mfumo wa Kiislamu, lakini bila shaka changamoto hiyo haikuwaathiri na wala haitawaathiri wananchi wa Iran katika siku zijazo. Nchi kadhaa za Magharibi zikiongozwa na Marekani, ziliitumia kadhia ya nyuklia kama wenzo wa kulishinikiza taifa la Iran. Maadui wa mfumo wa Kiislamu, kila mara wamekuwa wakitumia visingizio vya nyuklia katika kuhalalisha madai yao yasiyokuwa na msingi, ili kuweka vikwazo vipya dhidi ya taifa la Iran. Lakini viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kalibu ya mazungumzo na kundi la 5+1 na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA , wameilinda haki ya kimsingi ya nyuklia ya taifa la Iran, na kamwe hawakutetereka wala kuyumbishwa na mashinikizo na vitisho vya Wamagharibi. Kwa mujibu wa makubaliano ya kuzuia kuzalisha, kutumia na kusambaza silaha za nyuklia 'NPT', utumiaji wa nishati ya nyuklia kwa njia za amani ni haki ya mataifa yote likiwemo taifa la Iran na hakuna awezaye kuzuia haki hiyo. Uzoefu wa miaka 34 iliyopita unaonyesha kuwa, hakuna suala lolote lisilo la kimantiki lililowazuia wananchi wa Iran kupiga hatua za kimaendeleo. Aidha Ayatullah Khamenei amevitaja vikwazo kuwa ni changamoto nyingine inayoikabili Iran. Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kisingizio kinachotumiwa kuiwekea viwkazo Iran kidhahiri ni kadhia ya nyuklia, lakini sababu hasa ya suala hilo ni lengo la muda mrefu linalofuatiliwa na madola ya Magharibi. Ili kukabiliana na vikwazo hivyo, kumejitokeza harakati za ndani za wananchi ambazo zimeweza kufanikisha urutubishaji wa madini ya urani kwa asilimia ishirini inayotakiwa kwenye kinu cha nyuklia cha kiutafiti cha Tehran. Nchi ambazo leo hii zinaiwekea vikwazo Iran, zenyewe zinakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi. Leo hii kunashuhudiwa kwenye miji mbalimbali ya Ulaya na baadhi ya miji ya Marekani, wananchi wakikabiliwa na matatizo ya kiuchumi na wamekuwa wakijitokeza mabarabarani wakilaani na kupiga nara dhidi ya sera za kiuchumi za nchi hizo. Mara baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, nchi za Magharibi zilifanya njama kadhaa za kuwapambanisha wananchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini njama hizo ziligonga mwamba kutokana na wananchi wa Iran kuwa macho. Kwa maelezo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kuwapambanisha wananchi na mfumo, ni lengo kuu la vikwazo, amma kile kinachoonekana leo hii kwenye medani muhimu za mapinduzi ya Kiislamu kama vile maandamano ya kila mwaka ya tarehe 22 Bahman ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kumiminika kwa wingi wananchi kwenye chaguzi mbalimbali, ni ushahidi tosha wa kuwepo umoja na mshikamano baina ya wananchi na Mfumo. Kupigwa hatua za maendeleo hapa nchini na kujitokeza wananchi kwenye medani, ikiwemo kujitokeza kwa wingi kwenye chaguzi mbalimbali, ndiyo sababu kuu ya maadui kuingiwa na hasira na kuwa dhidi ya wananchi na taifa la Iran.
1200602
captcha