IQNA

Imam Khamenei:Mitazamo ya Marekani inakinzana kuhusu mauaji ya watu wasio na hatia

14:06 - April 18, 2013
Habari ID: 2520698
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Marekani ina mtazamo unaokinzana kuhusu mauaji ya watu wasio na hatia.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumatano hii alionana na majimui ya makamanda, maafisa walioteuliwa kwa ajili ya mkutano huo na wajumbe wa vituo vya basiji vya miji ya taasisi ya kijeshi na vile vile familia kadhaa za maafisa hao wa kijeshi kwa mnasaba wa kukakaribia Farvardin 29 (Aprili 18) ambayo ni Siku ya Jeshi nchini Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni fakhari ya taifa na ni jeshi la wananchi lililopambika kwa sifa nzuri za kielimu, kiitikadi na lenye ubunifu wa kila namna na huku akiashiria jinsi kambi ya kibeberu inayoongozwa na Marekani isivyotumia mantiki katika mambo yake amesisitiza kuwa: Leo ustaarabu wa Magharibi umekaribia kusambaratika na kuporomka kabisa kutokana na kukosa mantiki, kuwa na migongano mingi, ubeberu na utumiaji mabavu na kutojali misingi ya kibinaadamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ambaye ndiye Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia pia sifa za kipekee za Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na jinsi jeshi hilo lilivyo la wananchi na kuongeza kuwa: Katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jeshi linapendwa, linaungwa mkono na kuheshimiwa mno na wananchi si kwa sababu ya kutumia mabavu na kufanya ubeberu, bali kutokana na kujitoa muhanga na kupigana jihadi kwa ajili ya kulilinda taifa.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema kuhusu kupambika jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sifa za kielimu kwamba: Maendeleo na upana wa kazi za kielimu na kiutafiti zinazofanywa na vikosi vya ulinzi nchini likiwemo jeshi katika upande wa viwanda vya kijeshi na elektroniki ni ya kupigiwa mfano na ya kustaajabisha ambayo hayawezi kabisa kufananishwa na jinsi hali ilivyokubwa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu bali na hata katika miaka ya awali ya Mapinduzi hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia sifa ya kidini na kiimani iliyojikita ndani ya jeshi hilo na kusema kuwa: Kufanya kazi kwa kuamini kuwa ni kutekeleza jukumu la kidini na kutiwa nguvu moyo wa kidini na kimapinduzi jeshini kumelifanya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa jeshi lilipevuka kiimani na kushikamana vilivyo na itikadi na matukufu ya kidini.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Bila ya shaka yoyote jeshi lililopambika kwa sifa kama hizo huibuka na ushindi katika mtihani wowote ule.
Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja uzoefu lilio nao jeshi la Iran kutokana na ushindi mkubwa lilioupata katika vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran) kuwa ni sifa nyingine bora ya jeshi hilo na kusisitiza kuwa: Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanya kazi kubwa na muhimnu mno katika operesheni mbali mbali za kipindi chote cha vita vya kujihami kutakatifu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kuwa, maafisa hao wa kijeshi wanapaswa kujivunia kuwa kwao wanajeshi na waongeze hima katika kulinda na kutia nguvu sifa bora waliyo nayo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria jinsi vikosi vya ulinzi vya Iran vilivyo na sifa zinazotofautiana kabisa na majeshi mengine duniani na kuongeza kuwa: Jeshi la Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) na Jeshi la Basiji ni utamaduni, aidiolojia na fikra mpya ambayo taifa la Iran imeionesha kwa walimwengu na ni kigezo kizuri na mfano bora katika kukabiliana na misimamo ya kikoloni na kibeberu ya majeshi ya madola ya kibeberu duniani.
Vile vile amezungumzia tabia ya kibeberu ya majeshi ya kambi ya kibeberu hasa Marekani na kusema kuwa: Majeshi ya madola hayo yanapoingia katika sehemu yoyote ile duniani huwa ni chanzo cha ufisadi wa kimaadili na mashinikizo makubwa pamoja na maudhi na mauaji dhidi ya wakazi wa maeneo hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia madai ya Wamarekani wanaodai kwamba wanapinga silaha za mauaji ya umati na kuongeza kuwa: Kinyume kabisa na madai yao hayo, kila leo ndege zisizo na rubani za Marekani zinawaua kwa umati watoto wadogo, wanawake na watu wasio na hatia huko Afghanistan na Pakistan huku magaidi wanaoungwa mkono wazi wazi na kwa siri na Marekani nao wakiuwa watu katika nchi za Iraq na Syria.
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha pia migongano iliyopo katika maneno na vitendo vya Marekani na kuongeza kuwa: Marekani na madola mengine yanayodai kutetea haki za bindaadamnu duniani yananyamazia kimya mauaji wanayofanyiwa wananchi wasio na hatia wa Pakistan, Afghanistan, Iraq na Syria lakini baada ya kutokea miripuko michache tu huko Marekani dunia nzima imekumbwa na makelele yasiyo na kifani.
Aidha amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na kufuata kwake mantiki ya Kiislamu inapinga na kulaani mripuko na mauaji ya aina yoyote yale ya watu wasio na hatia iwe ni wananchi wa Boston Marekani au wananchi wa Pakistan, Afghainstan, Syria na Iraq.
Ameongeza kuwa: Vitendo vya Marekani na madola mengine yanayodai kutetea haki za binaadamu vinakinzana kuhusiana na mauaji ya watu wasio na hatia na ni kwa sababu hiyo ndio maana sisi tunaamini kuwa Marekani na kambi iliyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, haitumii mantiki.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ustaarabu wa nchi za Magharibi uko katika hatari ya kusambaratika na kuporomoka kabisa kutokana na kuweko migongano yote hiyo na kutotumia kwake mantiki na kutumia kwake mabavu na ubeberu na kutojali kwake misingi ya kibinaadamu.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amehoji akisema: Hii ni mantiki ya namna gani ambayo wakati Wamarekani wanapoua watoto wadogo na wanawake huko Afghanistan na Pakistan, huku magaidi wanaoungwa mkono na Marekani, Magharibi na Wazayuni wakifanya mauaji ya kutisha katika nchi za Iraq na Syria, huwa hakuna tatizo lolote na jambo hilo linaonekana la kawaida lakini wakati unapotokea mripuko tu nchini Marekani au katika nchi fulani ya Magharibi, dunia nzima inalazimishwa kulipa hasara za mripuko huo?
Amesisitiza kuwa: Tabia na dhati ya Marekani na nchi za Magharibi ya kujiona bora kuliko watu na mataifa mengine yote, ndiyo itakayopelekea kusambaratika kwao na kuzidi kupoteza nguvu zao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria fikra za kimantiki zinazotawala katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Fikra hizo za kimantiki ndizo zinazoweka msingi wa ustaarabu mkubwa na wa kudumu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amewashukuru wake, familia na wana wa maafisa wa kijeshi kutokana na kujitolea kwako katika mambo mengi na kuwa pamoja na maafisa hao wakati wote na kuongeza kuwa: Familia za maafisa wa jeshi nchini zinapaswa kujivunia na kuona fakhari kwamba wapendwa wao wanatumika jeshini.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Meja Jenerali Salehi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ametoa ripoti kuhusu uwezo wa jeshi hilo na kuwa kwake tayari wakati wote kulinda vilivyo mipaka ya nchi.
Mwanzoni mwa mkutano huo, baadhi ya majeruhi wa vita wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameonana kwa karibu na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
1214348
captcha