IQNA

Siku ya Naqba, siku ya kukumbuka kukaliwa kwa mabavu Palestina

14:48 - May 16, 2013
Habari ID: 2534378
Jana Jumatano tarehe 15 Mei, ilikuwa siku ya kukumbuka kutimia miaka 65 tangu ardhi za Palestina zilipokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel, siku inayojulikana kama 'Siku ya Naqba.'
Miaka 65 iliyopita kama leo, Wazayuni kwa kuungwa mkono na Uingereza na baada ya kupita karne kadhaa, hatimaye walifanikisha njama yao ya kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Kufuatia kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na Wazayuni mnamo Mei 15 mwaka 1948, siku ambayo ilipewa jina la 'Siku ya Naqba,' kulianza operesheni za kuwafukuza taratibu mamia ya maelfu ya Wapalestina kutoka katika ardhi yao ya asili, kiasi kwamba hadi sasa mamilioni ya Wapalestina wameshafukuzwa kwenye nchi yao na sasa wanaishi kama wakimbizi katika sehemu tofauti za dunia huku wakikabiliwa hali ngumu.Ijapokuwa Wapalestina wanaiita siku hii kuwa 'Siku ya Naqba ya Taifa la Palestina'lakini tunaweza kusema kuwa, siku hii ni siku ya Naqba kwa mataifa ya Waarabu, na kwa kuzingatia madhara ya kuasisisiwa Israel kwenye ardhi zilizoghusubiwa za Palestina, siku hii pia ni nakama na maafa makubwa kwa jamii ya mwanadamu. Ukweli ni kuwa, maafa hayo ni doa jeusi la fedheha lilioikumba jamii na mfumo wa kimataifa, na hata baada ya kupita miaka 65 hadi hivi sasa doa hilo bado halijafutika. Hii ni kwa sababu wakimbizi wa Kipalestina ambao sasa wanakadiriwa kufikia milioni 5, bado wanasubiri siku ardhi yao itakapokombolewa ili warejee katika nchi yao. Hii leo kadhia ya wakimbizi wa Kipalestina ambayo ni sehemu tu ya mgogoro wa Palestina, inayosisitizwa pia na azimio nambari 194 la Umoja wa Mataifa, bado ni changamoto kubwa kwa jamii ya kimataifa. Hasa kwa kuzingatia kuwa, mgogoro wa Palestina hauwezi kutatuliwa bila kutatuliwa suala hilo, kwa sababu wakimbizi wa Palestina wanaishi katika nchi tofauti kwa tabu, majonzi na kudharauliwa. Hata hivyo, ukweli ni kuwa chanzo cha kukaliwa kwa mabavu Palestina na Israel ni matokeo ya njama zilizoratibiwa mwaka 1897 huko Bal Uswizi, na kuandaa mazingira ya kuasisisiwa kwa awamu Israel, kutokana na usimamizi wa Uingereza kwa Palestina na kutangazwa Azimio la Balfour mwaka 1917. Mwenendo huo uliendelea hadi Novemba 29 mwaka 1947 ambapo Umoja wa mataifa ulipitisha azimio nambari 181 kuhusu Palestina. Kwa mujibu wa azimio hilo, Palestina iligawanywa kati ya Waarabu na Wayahudi. Nchi 23 ikiwemo Marekani, Uingereza na nyinginezo za Ulaya zilipigia kura ya ndio azimio hilo. Azimio nambari 181 lilipitishwa mwaka mmoja kabla ya kujiri tukio chungu la kughusubiwa ardhi za Palestina, na ni ushahidi unaothibitisha njama iliyoratibiwa kimataifa ya kuasisiwa Israel na kuiondoa Palestina kutoka katika moyo wa ulimwengu wa Kiislamu. Tangu Mei 15 mwaka 1948 ambapo Israel ilitangazwa rasmi kuwepo kwake hadi leo, kila mwaka 'Siku ya Naqba' huadhimishwa, huku fungu la Wapalestina likiwa si jingine ghairi ya machungu, mateso, ukimbizi na kuishi ugenini. Kwa kuzingatia hali hiyo, kimya cha ulimwengu wa Kiislamu mkabala na mgogoro wa Palestina, ni suala lisilokubalika hata kidogo. Kama wanavyosema wachambuzi wa masuala ya kieneo, hii leo kadhia ya Palestina ni mtihani mkubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu, na kwa kuzingatia uwezo wao, iwapo nchi hizo zitasimama kidete dhidi ya uvamizi wa Wazayuni, basi zitakuwa zimewapa somo Wamagharibi na madola ya kibeberu. Lakini iwapo hazitofanya hivyo na kuendelea kukaa kimya, basi zinapaswa kusubiri kuvamiwa na Wamagharibi kutokea kila upande, na pengine migogoro na ukosefu wa amani unaoshuhudiwa sasa huko Iraq, Syria, Yemen na katika nchi nyingine za Kiislamu ni sehemu tu ya uvamizi huo.

1228777
captcha