Dakta Sayyid Muhammad Husseini, Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran amesema kuwa, kushikamana na Qur’ani Tukufu, ndiyo njia pekee ya kuwaokoa Waislamu kutokana na njama za maadui duniani.
Dakta Husseini aliyasema hayo hapo jana kando ya Mashindano ya 31 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu yanayoendelea hapa mjini Tehran sambamba na kukumbuka miaka 24 tangu kufariki dunia Imam Khomein (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Husseini amesema kuwa, wageni mbalimbali waliofika nchini hapa kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo, watapata kunufaika na historia ya shakhsia huyo na nafasi yake muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Ameongeza kuwa, uelewa sahihi wa Imam kuihusu Qur’ani, ulileta mabadiliko muhimu katika jamii na kwamba, hata taifa hili la Kiislamu limesimama kwa kutegemea mafundisho sahihi ya Kitabu hicho Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu. Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu wa Iran amesema kuwa, ikiwa mwanadamu atashikamana na njia ya Mwenyezi Mungu, basi atapata msaada na ushindi kutoka kwa Allah na kuwa hakuna mtu yoyote atakayeweza kumshinda.
1237897