Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, maonyesho hayo yataanza Julai 5 katika sherehe itakayohudhuriwa na rais anayeondoka wa Iran Mahmoud Ahmadinejad. Sherehe ya kufunga maonyesho hayo imepangwa kuhudhuriwa na rais-mteule wa Iran Sheikh Hassan Rohani.
Hayo yamedokezwa na Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Iran Dkt. Sayyed Mohammad Husseini ambayo ameongeza kuwa nchi 30 zitashiriki katika maonyesho hayo ya kimataifa ya Qur’ani. Maonyesho ya Kimataifa ya Qur’ani Tehran huanza siku chache kabla ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuendelea hadi siku za mwisho za mwezi huu mtukufu.
Lengo la maonyesho hayo ni kuimarisha na kuboresha ufahamu wa Qu’rani Tukufu. Kauli mbiu ya maonyesho ya mwaka huu ni ‘Mfumo wa Maisha kwa Mujibu wa Qur’ani’.
Kwingineko Waziri wa Utamaduni na Miongozo wa Kiislamu nchini Iran amesema nchi za Magharibi haziwezi kustahamili ‘sauti ya haki’ na ndio sababu zimepiga marufuku matangazo ya radio na televisheni za Iran katika satalaiti.
Dkt. Sayyed Mohammad Husseini ameongeza kuwa hatua ya Wamagharibi ya kupiga marufuku radio na televisheni za Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB ni ishara ya mafanikio na ushawishi wa kanali hizo kwa walimwengu.
Amesema upigaji marufuku kanali za Iran ni jambo linaloashiria undumakuwili wa wamagharibi kuhusu madai yao ya eti kutetea uhuru wa kujieleza.
Dkt. Husseini amesema, Iran itachukua hatua za kisheria dhidi ya uamuzi wa mashirika ya satalaiti kukata kanali za IRIB.
Juni 19, shirika la Intelsat lilisema kuanzia Julai Mosi halitatoa huduma kwa kanali za Iran kwa kisingizio kuwa shirika hilo linatekeleza vikwazo vya Marekani dhidi ya mkurugenzi mkuu wa IRIB.
Utawala wa Kizayuni wa Israel kupitia makundi yake ya lobby huko Marekani, umeshinikiza mashirika ya satalaiti duniani kuzuia matangazo ya radio na televisheni za Iran. Ni wazi kuwa nchi za Magharibi zinazuia vyombo vya habari vya Iran ili kuzima sauti ya haki kuwafikia walimwengu.
1251429