
Sheikh Ahmed Al-Tayyib, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kiislamu, alimwambia Rais wa Italia, Sergio Mattarella, katika mkutano uliofanyika Roma, kuwa ni muhimu kwa taifa hilo la Ulaya kulitambua rasmi Taifa la Palestina.
Mkutano huo ulifanyika pembeni ya mkutano wa kimataifa wa “Dare for Peace” ulioandaliwa na Jumuiya ya Sant’Egidio.
Sheikh Al-Tayyib alionesha kuthamini msimamo wa wananchi wa Italia na mshikamano wao na Wapalestina, pamoja na maandamano yao makubwa kupinga mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Gaza.
“Tunathamini msimamo wa kimaadili ulioonyeshwa na wananchi wa Italia, na tunatarajia Italia itaungana na mataifa mengine yaliyolitambua rasmi Taifa la Palestina, ikiwa ni hatua kuelekea kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina lenye mji wa Quds Mashariki kama mji mkuu wake,” alisema Imam Mkuu huyo.
Aidha, alisisitiza kwamba Al-Azhar itaendelea kusimama kwa dhati katika kuimarisha amani, ujumbe wa msingi wa Uislamu, pamoja na kupambana na upotoshaji kuhusu dini kupitia majadiliano na ushirikiano na taasisi za kimataifa za kidini na kitamaduni.
Akikumbusha kutiwa saini kwa Hati ya Udugu wa Kibinadamu mwaka 2019 katika Abu Dhabi akiwa na marehemu Papa Francis, Sheikh Al-Tayyib alisema mpango huo unaendelea kuimarisha mazungumzo ya baina ya dini na juhudi za kupambana na ubaguzi, misimamo mikali, na hotuba za chuki.
Rais Mattarella alisifu juhudi za Sheikh Al-Tayyib katika kueneza amani na uhusiano wake wa karibu na Papa Francis, akieleza kuwa Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni “nguzo muhimu katika kustawisha amani ya kimataifa na mazungumzo ya kidini.”
Pia aliipongeza hotuba ya Sheikh Al-Tayyib katika ufunguzi wa mkutano huo akisema imejaa “ujumbe wenye maana na mapendekezo ya vitendo ya kuleta amani.”
Pande zote mbili zilijadili kuendeleza ushirikiano kati ya Al-Azhar, Baraza la Wazee wa Kiislamu na Kanisa Katoliki, hususan katika mipango ya kuwawezesha wanawake na kushirikisha vijana katika ujenzi wa amani, huku zikisisitiza dhamira ya pamoja ya kuendeleza mazungumzo ya baina ya dini na kuimarisha maisha ya kuheshimiana na kuishi kwa amani.
3495193