IQNA

Arubaini ya Imam Hussein AS

17:40 - December 13, 2014
Habari ID: 2617894
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Takribani miaka 1375 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) akiwa na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria.

Majlisi za siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala.

Zimepita siku arubaini tokea lijiri tukio la Ashuraa. Hii ni Ashura ya damu na mwamko, ni Ashuraa ya vichwa vilicyochinjwa na viwiliwili vilivyodungwa mishale na watoto walioadhibiwa! Ni Arbaeen inayosimulia namna hema zilivyoteketezwa moto na makatili walivyowaua shahidi watu wasiokuwa na hatia. Ni siku arubaini ambapo wana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW walikuwa wakihangaika katika jangwa lenye masaibu mengi huku wakiwa na majeraha. Mtawala wa zama hizo, Yazid ibn Muawiya alifurahia hali hiyo akiwa na dhana potofu kuwa ametekeleza haki. Hata hivyo, ushujaa na kusimama kidete Bibi Zainab SA na Imam Sajjad AS ni jambo ambalo lilisambaratisha njama chafu ya Yazid na vibaraka wake. Hivi sasa walimwengu wote wanakiri kuwa Imam Hussein AS, Bwana wa Mashahidi ndiye aliyepeta ushindi wa milele.
Ahul Bayt wa Mtume SAW ni kati ya vizito viwili ambavyo Mtume Muhammad SAW aliuachia Umma wa Kiislamu ili viwe kinga ya kutotumbukia katika mkondo potofu. Mtume SAW alisema: "Mimi ninawaachia vizito viwili vyenye thamani ambavyo iwapo mtashikamana navyo kamwe hamtapotea; navyo ni Kitabu Cha Mwenyezi Mungu na Itrah yangu, ambao ni Ahul Bayt, au Watu wa Nyumba Yangu."
Wakati bendera ya mwamko wa Aba Abdillah AS ilipoanguka ikiwa mikononi mwa mbeba bendera wake yaani Hadhrat Abbas bin Ali AS na kichwa kitukufu cha Imam Hussein AS kikaanguka chini mbele ya Ahlu Bayt wake kikiwa kimedungwa kwa mishale, Yazid na vibaraka wake walidhani kuwa wamefanikiwa kuwapokonya Waislamu moja kati ya vitu viwili vyenye thamani na kwamba kwa hatua yao hiyo wangeweza kupotosha Qu'rani ambayo ni kati ya vizito viwili vilivyoachwa na Mtume SAW. Hata hivyo, kwa irada ya Mwenyezi Mungu, damu ya Hussein AS daima iko katika mishipa ya Waislamu wanaofuata haki na wapenda uadilifu kote duniani.
Arbaeen ya Imam Hussein AS daima imekuwa ikikumbukwa na Waislamu hasa wa madhehebu ya Shia. Wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume SAW, tokea mwaka wa kwanza wa kuuawa Shahidi Imam Hussein AS wamekuwa wakifanya ziara katika Haram yake takatifu. Sunna hii ingali inaendelezwa na hadi leo tunashuhudia namna ambavyo mamilioni kwa mamilioni ya Waislamu kutoka kote duniani wanavyojumuika katika Haram Takatifu ya Imam Hussein AS ili watangaze kuwa wao ni wafuasi wa njia ya Hussein na wako chini ya kivuli cha Wilaya yake, na kwamba hawatasalimu amri mbele ya dhulma na kwamba watajitolea muhanga katika njia hiyo ya kuutetea Uislamu.
Jabir bin Abdullah Ansari, Sahaba wa Mtume alikuwa mfanya ziara wa kwanza aliyefika Karbala katika siku ya Arbaeen. Pamoja na kuwa alikuwa kipofu, akiwa amenadamana na Atiya Bin Saeed Al-Kufi Mwanazuoni na mfasiri wa Qur'ani, walifanya ziara katika kaburi takatifu la Imam Hussein AS. Attiya Al-Kufi amenukuliwa akisema: "Nikiwa pamoja na Jabir tumewasili Karbala kwa lengo la kuzuru kaburi la Imam Hussein AS...Punde baada ya kuwasili Jabir aliniambia hivi: 'Nipeleke katika kaburi la Hussein.' Mimi niliushika mkono wake na kuuweka juu ya kaburi. Hapo Jabir alianguka juu ya Kaburi na kuzimia. Nilimwaga maji kwenye uso wake na alipopata fahamu alisema hivi mara tatu mfululizo..: 'Ya Hussein' kisha akaendelea kusema: 'Ewe Hussein mbona haunijibu?" Kisha akasema: 'Ni vipi utaweza kunijibu wakati mishipa ya koo lako imekatwa na kichwa chako kutenganishwa na mwili?' Nashuhudia kuwa wewe ni mwana wa Mtume wa Mwisho na Bwana wa Waumini... Sala, Salamu na Radhi za Allah SWT ziwe juu yako."

Katika nyaraka za kale zaidi za Kiislamu, kumetajwa suala la kumzuru Imam Hussein AS katika Siku ya 'Arbaeen'. Ushahidi muhimu zaidi kuhusu hili ni Riwaya ya Imam Askari AS ambaye alisema: "Ishara za muumini ni katika vitu vitano: Kusali rakaa 50 kila siku -ambazo zinajumuisha sala za faradhi na nawafil-, Ziara ya Siku ya Arbaeen, Pete katika mkono wa kulia, kusujudu katika udongo na kusema Bismillahir Rahmani Rahim kwa sauti katika sala."
Katika riwaya nyingine imenasihiwa kuwa, watu ambao katika siku ya Arbaeen hawawezi binafsi kufika Karbala wasome Ziara ya Arbaeen kwa mbali. Jambo hili linaashiria umuhimu wa Siku ya Arbaeen na pia ni kumbukumbu ya Kamusi ya Kiislamu kuhusu utamaduni wa kupinga dhulma katika Siku ya Ashura. Kutoka Siku ya Ashura hadi Arbaeen kuna siku arubaini. Katika siku hizo arubaini ni Bibi Zainab SA ambaye kwa busara na ujasiri sawa na wa Imam Ali AS alipelekea kuambulia patupu Yazid katika ndoto yake ya kuibuka mshindi. Hii ni kwa sababu Bibi Zainab SA aliendelea kuinua bendera ya harakati ya Imam Hussein AS na ndio sababu hadi leo bendera hiyo ingali inapepea kwa nguvu. Ni Zainab SA ambaye alikuwa katika majonzi na kutokwa na machozi kutoka siku ya Ashura hadi Arbaeen ambapo kwa njia hiyo aliweza kusambaza ujumbe wa kudhulumiwa na kutetea haki Imam Hussein AS. Hotuba kali alizotoa Bibi Zainab zilitikisa kasri ya kila dhalimu na kuwavutia mamilioni ya watu kila mwaka kuelekea katika jangwa la Karbala.
Mbali na sifa zake za kipekee pamoja na fadhila alizokuwa nazo Bibi Zainab SA kutokana na kuzaliwa katika familia ya Wahyi, pia alikuwa na nafasi muhimu sana katika kufanikisha Harakati ya Ashura na mwamko wa Imam Hussein AS. Baada ya tukio chungu la Ashura, alichukua nafasi ya mlezi wa mateka na kumlinda Imam Sajjad AS ili asikabiliwe na hatari. Kutokana na kustahamili kwake masaibu, aliweza kuipatia ushindi kamili harakati ya kimapinmduzi ya Imam Hussein AS. Katika kutekelelza majukumu yake, Bibi Zainab SA alisimama kidete na kwa ushujaa ili kuhakikisha kuwa hakungekuwepo upotofu katika Uislamu, Sunna ya Mtume SAW na Mapinduzi ya Karbala.
Wakati msafara wa mateka wa Karbala ulipowasili Kufa, kundi la kwanza la watu waliokuwa na furaha walienda kuwapokea mateka hao ambao walijumuisha wanawake, watoto na askari. Lakini Bibi Zainab SA kwa hotuba yake yenye kubainisha na nzito alibadilisha hali hiyo na punde watu wa Kufa wakazama katika majonzi na maombolezo. Bibi Zainab katika sehemu ya hotuba yake alisema: 'Enyi watu waovu, wenye kuhadaa na wasioaminika....!Ni vipi mumemua kipenzi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW na Bwana wa Vijana wa Peponi? Yeye ndiye yule yule ambaye aliwapa hifadhi wakati wa vita na wakati wa amani alikuwa chanzo cha utulivu wenu. Je, mnajua ni vipi mlivyomuumiza roho Mtume na ni vipi mlivyovunja ahadi?"
Kwa maneneo mazito ya Bibi Zainab SA idadi kubwa ya watu wa Kufa walitambua kina cha dhambi zao. Aidha Bibi Zainab SA alipofika katika Kasri ya mtawala Obaidullah ibn Ziad huko Kufa, mtawala huyo alimkejeli sana na msafara wake. Hapo Bibi Zainab akatoa hotuba ambayo ilipelekea kusambaratika njama za Obaidullah ambaye alikuwa na nia chafu ya kupotosha utambulisho wa mwamako wa Imam Hussein AS. Mtawala wa Kufa alidhalilika kutokana na hotuba nzito iliyotolewa na Bibi Zainab SA na hivyo akaona kuwepo mateka hao hapo ni tishio kwake. Kwa hivyo aliamuru kuwa wapelekwe haraka iwezekanavyo katika makao makuu ya Khalifa wa zama hizo huko Sham.
Wakati msafara wa wafungwa ulipowasili Sham, wakaazi wa mji walikuwa na furaha tele kwani kutokana na propaganda sumu za Yazid watu walikuwa na dhana potofu kuwa Bibi Zainab SA na wenzake walikuwa wapinzani wa kile kilichokuwa kikitajwa kuwa ni Khilafa ya Kiislamu na hivyo walisema ni haki yao kuwa mateka. Yazid aliitisha kikao cha maafisa wa utawala na kijeshi ambapo katika majlisi hiyo iliyojaa ghururi na kiburi alikuwa akiupiga kwa kijiti mdomo na meno ya Umam Hussein AS huku akisema: 'Laiti wakuu wa kabila langu ambao waliuawa katika vita vya Badr wangekuwa hapa ili waone namna sisi tulivyowaua wakuu wa Bani Hashim na hivyo kulipiza vita vya Badr....Bani Hashim walihadaa katika utawala kwani hakukuwa na malaika wala Wahyi..." Kwa maelezo hayo Yazid akiwa mlevi alibainisha wazi ukafiri wake kwa Mtume na dini ya Mwenyezi Mungu. Hapo Bibi Zainab SA alitoa hotuba iliyofichua mengi na hadhirina wakamkumbuka Imam Ali AS. Katika sehemu ya hotuba yake Bibi Zainab SA alisema: "Mwenyezi Mungu alisema kweli pale aliposema:... Kisha ulikuwa mwisho wa waliofanya ubaya ni kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia maskhara...(Surat Ar-Rum aya ya 10.) Ewe uliyezaliwa na Muawiya! Ingawa hali ya mambo imepelekea tuwe hivi tulivyo na hivyo kuzungumza mbele yako, nakuona ukiwa mtu duni wa kuzungumza naye kwani wewe una madhambi mengi na utapata adhabu ambazo hatuwezi kuzihesabu. Lakini nifanyeje? Mimi nina majonzi kutokana na vifo vya vipenzi vyangu...Ewe Yazid! Fanya uwezalo. Naapa kwa Mwenyezi Mungu hauwezi kuzima na kupotosha majina na Wahyi wetu....
Hotuba ya Bibi Zainab ilijaa hisia na ushujaa kiasi cha kumdhalilisha kabisa Yazid ambaye kutokana na kushindwa la kusema alitangaza kuwa muuaji wa Imam Hussein AS alikuwa ni Ibn Ziad mtawala wa Kufa.
Hotuba ya Bibi Zainab AS katika Majlisi ya Yazid na baada ya hapo hotuba ya Imam Sajjad AS ni hotuba ambazo zilibadilisha hali ya mambo mjini Damascus kwani haki iliwabainikia wananchi kwa namna ambavyo haikutarajiwa.
Naam, hivi ndivyo Bibi Zainab alivyotekeleza majukumu yake katika kufikisha ujumbe wa harakati ya Imam Hussein AS na hatimaye kwa ushindi na heshima aliwasili Karbala akiwa na majonzi ya kuwaomboleza vipenzi wake.
Leo wanaompenda Imam Hussein AS sawa na maadhimisho ya Arbaeen katika karne zilizopita wanafika Karbala wakiwa na majonzi makubwa. Wanatembea wiki kadhaa kwa miguu huku wakivumilia nyusiku zilizojaa baridi kali jangwani na hayo yote ni kwa ajili ya mapenzi yao kwa Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein AS. Mapenzi na mahaba haya ni ya kumzuru Bwana wa Vijana wa Peponi ambaye Mtume Mtume SAW alimtaja kuwa 'Safina ambayo itauokoa Umma na Mwanga wa kuwaongoza wanaadamu milele.'
Kwa hakika mjumuiko wa mamilioni kwa mamilioni ya Waislamu katika Siku ya Arbaeen ni dhihirisho la kuwa wanataka kuangamiza upotofu na batili huku wakiamrisha mema ili kuhakikisha kuwa Uislamu halisi ndio unaobaki. Msisimuko huu wa mapenzi makubwa kwa Imam Hussein AS ni ishara kuwa mashetani wa zama hizi nao wataambulia patupu katika njama zao na Uislamu halisi utaenea kote duniani.../mh

2617870

captcha