IQNA

Rouhani: Ugaidi hauna uhusiano na Uislamu

20:20 - January 27, 2015
Habari ID: 2771315
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa maafa makubwa yanayofanywa na makundi ya kigaidi kama lile la Boko Haram yanaathiri na kuumiza sana dhamira za wanadamu kote dunia.

Rais Rouhani ameyasema hayo Jumatatu mjini katika mazungumzo yake na balozi mpya wa Kenya mjini Tehran Bi Rukia Ahmed Subow na kusisitiza kuwa, mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji ushirikiano mkubwa wa nchi zote. Ameongeza kuwa inasikitisha kuona kwamba, makundi mengi ya kigaidi yanafanya shughuli zao kwa kutumia jina la Uislamu lakini matendo na mwenendo wao unapingana kikamilifu na misingi ya Kiislamu.

Rais Rouhani ameashiria harakati za kigaidi katika eneo al Mashariki ya Kati na Afrika na hali ya ukosefu wa amani inayosababishwa na maharamia katika pwani ya Somalia na akasema, kuna udharura wa kusaidiana katika masuala ya kiutamaduni, kisiasa na kipelelezi ili kuweza kung’oa kabisa mizizi ya ugaidi. Rais wa Iran amesema Kenya ni nchi muhimu na yenye taathira katika eneo la mashariki mwa Afrika na kuongeza kuwa, uhusiano wa Tehran na Nairobi umekuwa na umuhimu mkubwa siku zote kwa Jamhuri ya Kiislamu. Ameashiria pia nafasi muhimu ya kijiografia na uwezo wa kiuchumi wa Kenya na kusema, anataraji kuwa balozi mpya wa Kenya hapa nchini atasaidia kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili hususan katika nyanja za uchumi, sayansi na utamaduni.

Kwa upande wake balozi mpya wa Kenya mjini Tehran Bi Rukia Ahmed Subow amesema nchi yake ina hamu kubwa ya kustawisha zaidi uhusiano na Iran na kwamba iwapo hati za maelewano zilizotiwa saini baina ya pande hizo mbili zitatekelezwa, kiwango cha uhusiano wa nchi mbili kitaimarika zaidi.../mh

2766648

captcha